1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri: 'Siku ya Kuondoka' ndiyo leo

4 Februari 2011

Shinikizo la kumtaka Rais Hosni Mubarak aondoke madarakani limepamba moto, huku leo waandamanaji wakiitisha wanachokiita "Siku ya Kuondoka" na Marekani ikisemekana kuandaa mpango wa Mubarak kuondoka kabla ya Septemba.

https://p.dw.com/p/10Aaw
Waandamanaji wakikusanyika Tahrir
Waandamanaji wakikusanyika TahrirPicha: dapd

Siku ya 11 ya maandamano ya Wamisri kumshinikiza Rais Hosni Mubarak aondoke madarakani, na leo wameipa jina la "Siku ya Kuondoka", wakimaanisha kuwa ndiyo siku watakayomng'oa kiongozi huyo madarakani.

Tayari maelfu kwa maelfu wameshakusanyika kwenye uwanja wa al-Tahrir, ambapo baada ya sala ya Ijumaa wanapanga kuelekea kwenye kasri ya rais, iliyo umbali wa kilomita 12 kutoka hapo.

Wakati huo huo, wafuasi wa Mubarak wamepanga kile wanachokiita "Siku ya Utiifu", wakionesha uungaji mkono wao kwa kiongozi huyu wa miaka 82, ambaye katika mahojiano yake na mwandishi wa kituo cha televisheni cha Marekani cha ABC, Christiane Amanpour, yaliyorushwa usiku uliopita, amesema kwamba yuko tayari kuondoka wakati wowote, lau asingelikhofia kuiwacha nchi yake kwenye machafuko.

Hali ni shwari

Makamo wa Rais, Omar Suleiman
Makamo wa Rais, Omar SuleimanPicha: picture-alliance/dpa

Usiku wa kuamkia leo ulipita salama katika uwanja wa Tahrir, ikilinganishwa na machafuko ya juzi na jana, ambayo, kwa uchache yamegharimu maisha ya watu 10, na wengine zaidi ya 800 kujeruhiwa.

Machafuko hayo yalitokana na watu wanaoshukiwa kuwa ni wafuasi wa Mubarak na maafisa wa usalama wa serikali yake, kuwavamia waandamanaji kwenye uwanja huo.

Tayari, Waziri Mkuu Ahmed Shafiq ameshaomba radhi kwa matukio haya, akiahidi uchunguzi kufanyika na hatua kali kuchukuliwa dhidi ya waliohusika.

Kiasi ya wanajeshi 1,000 wamesambazwa katika eneo la katikati ya mji mkuu wa Cairo, ambapo wamekuwa wakikagua kitambulisho cha kila anayeingia kwenye uwanja wa Tahrir, ili kuepusha makabiliano kama ya juzi na jana.

Makamo wa Rais, Suleiman Omar, alisema hapo jana kwamba, serikali haitawalazimisha waandamanaji kuondoka, japokuwa inawashauri wasiendelee na maandamano yao.

Marekani na mpango wa Mubarak kuondoka

Rais Hosni Mubarak (kushoto) na Rais Barack Obama
Rais Hosni Mubarak (kushoto) na Rais Barack ObamaPicha: AP

Katika hatua nyengine, serikali ya Marekani, ambayo ni mshirika mkubwa wa utawala wa Mubarak, imeripotiwa kuanza mchakato rasmi wa kumshawishi kiongozi huyo aondoke madarakani, haraka iwezekanavyo.

Gazeti la New York Times limeripoti kwamba utawala wa Rais Barack Obama umeanza majadiliano na maafisa wa Misri, likiwemo jeshi, katika mpango utakaomfanya Mubarak amuachie madaraka Makamo wake, Omar Suleiman, kuongoza serikali ya mpito itakayowajumuisha wapinzani, kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia hapo mwezi Septemba.

Marekani inatiwa hofu na namna hali ya usalama inavyodhoofika nchini Misri, na japo haisemi wazi, lakini inaiona serikali ya Mubarak ikizidi kupoteza udhibiti wa mambo.

Mashambulizi dhidi ya waandamanaji, wanaharakati wa haki za binaadamu na waandishi wa habari wa vyombo vya kimataifa, kumeifanya Washington, ianze kuwa na sauti nyengine kwa Mubarak.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/DPA
Mhariri: Othman Miraji