Maafisa saba wa jeshi la Pakistan wauawa katika shambulizi
12 Mei 2024Jeshi la Pakistan limesema kuwa katika shambulio la kwanza, kifaa cha mlipuko kililenga gari la kikosi cha kutegua mabomu katika eneo la Datta Khel jimboni Waziristan, Kaskazini mwa nchi hiyo jana Jumamosi. Baada ya mlipuko huo, washambuliaji hao walifyatua risasi.
Soma pia:Mashambulio ya Pakistan yaua watu kadhaa Afghanistan
Wanajeshi watano wa vikosi vya usalama waliuawa, na wawili kujeruhiwa. Katika shambulio la pili, wanamgambo walivamia kituo cha ukaguzi katika eneo la Mir Ali na kuwaua wanajeshi wawili.
Mashambulizi ya kundi la Taliban yaongezeka nchini Pakistan
Pakistan imeshuhudia ongezeko la mashambulizi ya kundi la Taliban la nchi hiyo tangu wenzao katika upande wa Afghanistan waliponyakua mamlaka nchini Afghanistan mnamo mwaka 2021.
Soma pia:Taliban: Pakistan imefanya mashambulizi ya anga Afghanistan
Mashambulizi ya hivi karibuni zaidi yanajiri siku chache baada ya wanamgambo kulipua bomu katika shule ya wasichana iliyoko Kaskazini mwa Waziristan, eneo linalojulikana kuwa kitovu cha shughuli za wanamgambo wa makundi ya itikadi kali.