Taliban: Pakistan imefanya mashambulizi ya anga Afghanistan
18 Machi 2024Taliban imelaani mashambulizi hayo ya anga na kuyataja kuwa uchokozi unaoilenga Afghanistan.
Wanawake na watoto wauawa katika mashambulizi
Katika taarifa, msemaji wa kundi hilo Zabihullah Mujahid, amesema mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya wanawake watatu na watoto watatu katika wilaya ya Barmal jimboni Paktika huku wanawake wengine wawili wakiuawa katika shambulizi jingine katika jimbo la Khost.
Mashambulizi ni ukiukaji wa uhuru wa Afghanistan
Mujahid ameongeza kuwa mashambulizi kama hayo, ni ukiukaji wa uhuru wa Afghanistan na kuonya kwamba kutakuwa na athari mbaya.
Wakati huo huo, wizara ya ulinzi nchini Afghanistanimesema vikosi vya nchi hiyo vimelenga vituo vya kijeshi vya Pakistan katika maeneo ya mipaka kwa silaha nzito nzito bila ya kutoa maelezo zaidi.
Wakazi Kaskazini Magharibi mwa Pakistan wahamia maeneo salama
Maafisa wawili wa Pakistan wamesema kuwa makombora yaliorushwa na kundi hilo la Taliban, yalisababisha kujeruhiwa kwa watu wanne na kwamba baadhi ya wakazi katika eneo la Kaskazini Magharibi la Kurram, leo walikuwa wanahamia maeneo salama.
Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan yathibitisha kutokea kwa mashambulizi
Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imethibitisha kutokea kwa mashambulizi hayo na kuyataja kama operesheni ya kijasusi ya kukabiliana na ugaidi katika maeneo ya mipaka ndani ya Afghanistan na kwamba yalikuwa yanalenga kundi lililojitenga la Wataliban wa Pakistan.
Suluhisho la pamoja linatafutwa kukabiliana na ugaidi
Wizara hiyo pia imesema kwamba inaendelea kutafuta suluhisho la pamoja katika kukabiliana na ugaidi ili kuzuia makundi yoyote ya kigaidi kuhujumu uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.
Mashambulizi hayo yanatokea baada ya wanamgambo ambao hawakutambulishwa, kushambulia siku ya Jumamosi kambi ya jeshi katika mji wa Mir Ali ulioko katika mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa unaopakana na Afghanistan na kusababisha vifo vya wanajeshi saba wa Pakistan.
Pakistan yadai Afghanistan inaunga mkono ugaidi
Katika taarifa iliyotolewa kwa televisheni ya taifa, jeshi la Pakistan limesema wimbi la hivi karibuni zaidi la ugaidi linaungwa mkono kikamilifu na Afghanistan.
Hata hivyo halikutaja mashambulizi yoyote ya anga lakini limesema kuwa shambulizi hilo la siku ya Jumamosi lilifanywa na wapiganaji walio na makazi salama nchini Afghanistan.
Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari, alihudhuria mazishi ya wanajeshi hao na kuapa kulipiza kisasi.
Kundi jipya la wanamgambo ladai kuhusika na mashambulizi
Kundi jipya la wanamgambo la Jaish-e-Fursan-e-Muhammad limedai kuhusika na shambulizi hilo la Mir Ali wakati maafisa wa usalama wa Pakistan wanaamini kwamba kundi hilo linajumuisha Wataliban wa Pakistanna kundi lililoharamishwa la Tehrik-e-Taliban Pakistan ama TTP, ambalo mara nyingi huwalenga wanajeshi na polisi wa Pakistan.
Mashambulizi ya Jumatatu ni tukio wazi la kulipiza kisasi
Muhammad Ali, mtaalamu wa masuala ya usalama mwenye makao yake mjini Islamabad, amesema kanali luteni mmoja wa jeshi ni miongoni mwa wale waliouawa Mir Ali na kwamba mashambulizi hayo ya leo ni tukio wazi la kulipiza kisasi linalokuja ndani ya masaa 24 ya onyo la Zardari.