1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Maafisa Korea Kusini wajaribu kumkamata Rais Yoon

Sylvia Mwehozi
3 Januari 2025

Maafisa nchini Korea Kusini wamefanikiwa kuingia katika makazi ya rais mapema leo Ijumaa, wakijaribu kumkamata kiongozi aliyeondolewa madarakani Yoon Suk Yeol.

https://p.dw.com/p/4omEH
Seoul 2025 | Korea Kusini
Maafisa wakijaribu kuingia ndani kumkamata rais YoonPicha: Yao Qilin/Xinhua/AP/picture alliance

Maafisa nchini Korea Kusini wamefanikiwa kuingia katika makazi ya rais mapema leo Ijumaa, wakijaribu kumkamata kiongozi aliyeondolewa madarakani Yoon Suk Yeol, wakati wafuasi wake wakiendelea kupiga kambi nje ya makazi hayo.

Maafisa kutoka ofisi ya kupambana na rushwa ya CIO, waliingia kwenye makazi hayo kupitia ulinzi mzito katika harakati za kumkamata Yoon anayechunguzwa kufuatia hatua yake ya muda mfupi ya kutangaza sheria ya kijeshi.

Yoon, ambaye tayari aliondolewa madarakani na wabunge, atakuwa rais wa kwanza aliyekuwa mamlakani kukamatwa katika historia ya Korea Kusini.

Seoul 2025
Umati wa wafuasi wa Rais Yoon waliopiga kambi nje ya makazi yakePicha: Ahn Young-joon/AP/dpa/picture alliance

Shirika la habari la Yonhap limeripoti kwamba maelfu ya maafisa polisi wamesambazwa katika mitaa ya kuelekea makazi hayo kufuatia makabiliano yaliyotokea siku ya Alhamis kati ya wafuasi wa kiongozi huyo na wapinzani wake.

Yoon amekuwa akijificha katika makazi hayo tangu mahakama ilipoidhinisha waranti ya kukamatwa kwake mapema wiki hii, akiapa "kupambana" na mamlaka zinazotaka kumhoji juu ya jaribio lake lililoshindwa la kutangaza sheria ya kijeshi.

Kiongozi huyo aliyekumbwa na msukosuko, alitangaza sheria hiyo mnamo Desemba 3, hatua iliyosababisha kuondolewa kwake mamlakani na kukabiliwa na kukamatwa, kufungwa au katika hali mbaya zaidi adhabu ya kifo.

Bado haikuwa wazi ikiwa idara ya usalama wa rais ambayo bado inamlinda Yoon kama itaafiki waranti ya kumkamata. Hapo awali, maafisa wa timu ya usalama wake walikuwa wamezuia jaribio la uvamizi wa polisi katika makazi ya rais.

Seoul | Rais Yoon Suk-yeol
Rais aliyeondolewa madarakani Yoon Suk YeolPicha: South Korean Presidential Office/Getty Images

Baada ya makabiliano ya Alhamis, baadhi ya wafuasi kindakindaki wa Yoon akiwemo nyota wa mtandao wa Youtube mwenye msimamo mkali na wachungaji wa kikristo, waliendelea kupiga kambi nje ya makazi yake usiku kucha wakisali. Wananadai kuwa waranti ya kumkamata kiongozi huyo "ni batili".

Soma: Chama tawala Korea Kusini chaahidi kupinga kumuondoa rais

Timu ya mawakili wanaomtetea Yoon iliwasilisha hoja za mapingamizi katika mahakama ya katiba kuzuia waranti na kuitaja kuwa ni "kinyume na sheria na batili".

Lakini mkuu wa ofisi ya CIO, Oh Dong-Woon alionya kwamba mtu yeyote atakayejaribu kuzuia mamlaka kumkamata kiongozi huyo huenda akashitakiwa.

Sambamba na waranti ya kumkamata, mahakama ya Seoul pia imetoa waranti ya upekuzi katika makazi yake binafsi na maeneo mengine.