M23 yakubali kuondoka kwa utaratibu mashariki mwa DRC
13 Januari 2023Waasi wa M23 wamekubali kuendelea kuondoka kwa utaratibu kwenye maeneo yaliyodhibitiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kulikogubikwa na machafuko. Msuluhishi wa Afrika Mashariki kwenye mzozo kati ya waasi hao na serikali Uhuru Kenyatta amesema hayo jana baada ya kukutana na viongozi wa M23 katika mji wa Mombasa nchini Kenya, hii ikiwa ni kulingana na taarifa iliyotolewa na ofisi yake. Sehemu ya taarifa ya Kenyatta imesema, pamoja na hatua hiyo inayolenga kuonyesha nia njema kuelekea kupata suluhu ya mzozo katika jimbo la Kivu Kaskazini, viongozi hao wamesema watazingatia usitishaji wa mapigano makali. Viongozi hao aidha wamekubali kuendelea kuheshimu na kushirikiana na jeshi la kikanda la Afrika Mashariki ambalo limeanza kuchukua udhibiti wa maeneo ambayo waasi hao wameondoka.