M23 wazidi kuteka maeneo mashariki ya Kongo
27 Januari 2023Mapigano hayo yaliyokuwa yakiendelea karibu na vijiji vya Kilolirwe na Burungu kwa siku mbili mfululizo, yalisambaa ghafla hadi katikati mwa mji wa Kitshanga ambako waasi hao wa M23 walifanikiwa kuuteka mji huo wa kibiashara.
Hali hiyo imeongeza wasiwasi mkubwa kwa maelfu wa raia waliokimbia makaazi yao wakielekea upande wa magharibi mwa wilaya hiyo yenye utajiri wa madini.
Soma zaidi: Rwanda yaishutumu Kongo kwa kukiuka makubaliano
Mkaazi mmoja aliyezungumza na DW kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema alishuhudia "maafa makubwa wakati mabomu yalipokuwa yakirushwa kuelekea nyumba zao na kuwajeruhi watu waliokuwa wakikimbia."
Mbunge kutoka mkoa wa Kivu Kaskazini, Muhindo Celce, alisema anasikitishwa nana kufungwa kwa barabara inayotoka Goma kuelekea masisi.
Wakimbizi waongezeka
Misururu ya wakimbizi imeshuhudiwa umbali wa kilomita 10 magharibi mwa mji wa Kitshanga.
Mwandishi wa DW katika eneo anaripoti kuwaona maelfu ya wakimbizi wanaoishi kwenye hali mbaya kutokana na ukosefu mkubwa wa chakula.
Soma zaidi: Rwanda yasema ndege ya kivita ya Kongo ilikiuka anga yake
Haya yanajiri siku mbili tu baada ya serikali ya Rwanda kudai kuwa ndege ya kivita ya Kongo iliruka katika anga yake bila idhini, tuhuma ambazo Kinshasa imezielezea kuwa ni "tangazo la vita" kati ya mataifa hayo mawili jirani.
Imeandikwa na Benjamin Kasembe, DW Goma