1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya: Serikali ya Tripoli kutoshiriki mazungumzo ya amani

19 Februari 2020

Serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imetangaza kuahirisha kushiriki katika mazungumzo ya amani ya Geneva yanayolenga kuokoa makubaliano hafifu ya kusitisha mapigano katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

https://p.dw.com/p/3XzVT
Libyen Angriff auf einen Hafen in der Nähe des Märtyrerplatzes
Picha: picture-alliance/AA/A. Kalabalik

Shambulizi hilo lilionekana kuwa la kwanza la aina hiyo dhidi ya bandari ya Tripoli tangu vikosi vya kijeshi vinavyomtii mbabe wa kivita, Khalifa Haftar, kuanza kuuvamia mji wa Tripoli takribani mwaka mmoja uliopita.

Taarifa kutoka serikali ya umoja wa kitaifa iliyoko mjini Tripoli, GNA, imesema kuwa mashambulizi ya ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yamerejelewa  na kwamba washambuliaji walilenga bandari ya Tripoli inayochukuliwa kuwa kiini cha maisha ya miji mingi nchini humo. Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa wanaahirisha kushiriki kwao katika mazungumzo hayo hadi wakati hatua kali zitakapochukuliwa dhidi ya washambuliaji na ukiukaji huo.

Serikali ya GNA imesema kuwa bila makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano ambayo yanaruhusu kurejea kwa wale waliopoteza makaazi yao na kuhakikisha kuweko kwa usalama katika mji huo mkuu na miji mingine, hakuna maana ya mazungumzo yoyote kwa sababu hakuna amani panapokuwa na mashambulizi ya mabomu.

Schweiz PK UN-Sonderbeauftragter für Libyen Ghassan Salamé
Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Libya- Ghassan SalamePicha: Reuters/D. Balibouse

Shirika la mafuta nchini humo limesema kuwa makombora yalirushwa mita chache kutoka kwa meli iliyokuwa imebeba mafuta na gesi na kusababisha kuondolewa kwa meli za mafuta kutoka eneo hilo na kufutilia mbali shughuli za kushusha bidhaa hizo.

Mpatanishi wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Ghassan Salame, amelitaja shambulizi hilo dhidi ya bandari ya Tripoli kuwa ''ukiukaji mkubwa'' wa makubaliano ya kusitisha mapigano. Salame amesema kuwa kumekuwa na visa zaidi ya 150 vya ukiukaji vilivyorekodiwa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalipotangazwa Januari 12. Ameongeza kuwa ghasia zinazoendelea nchini Libya zinafanya kuwa vigumu kuendelea na juhudi za Umoja wa Mataifa za kufikia makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano na suluhisho la kisiasa la mzozo huo na kwamba kadri ukiukaji huo unapotokea mara kwa mara, ni vigumu kufikiria kuhusu mazungumzo.

Libya imekumbwa na ghasia tangu mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani na kisha kuuawa kwa  Muammar Gadhaffi na taifa hilo limekuwa eneo la mapigano kati ya serikali pinzani zilizo na makao yao katika eneo la Mashariki na Magharibi ambazo zote zinaungwa mkono na mataifa ya kigeni kupata ushawishi wa kudhibiti raslimali nchini humo.