Umoja wa Mataifa na matumaini ya mazungumzo ya Libya
5 Februari 2020Ghassan Salame, anaeongoza tume ya Umoja wa Mataifa kwaajili ya Libya, amelalamika akisema vikwazo vya silaha vinavunjwa mtindo mmoja tangu utawala wa muda mrefu wa muimla Muammar Gaddafi ulipopinduliwa mwaka 2011.
Ameongeza kusema mkutano wa kimataifa ulioitishwa mjini Berlin mwezi uliopita ulilengwa kushadidia umuhimu wa kuheshimiwa makubaliano ya akuweka chini silaha.
Mazungumzo ya kuweka chini silaha yanaendelea mjini Geneva yanamulika kipengele cha kijeshi cha juhudi za kidiplomasia zilizolengwa kupunguza mivutano katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vurugu tangu mwongo mmoja uliopita.
Mahasimu wakuu wawakilishwa kwenye mazungumzo
Salame amesema mazungumzo kuhusu "kipengele cha kiuchumi yameanza mwezi uliopita mjini Tunis nchini Tunisia na yataendelea Jumapili inayokuja mjini Cairo.
Mazungumzo kuhusu kipengele cha kisiasa yamepangwa kuitishwa wiki mbili kutoka sasa, anasema.
Mahasimu wawili wakubwa, waziri mkuu Fayez Sarraj na jenerali Khalifa Haftar anaedhibiti sehemu kubwa ya ardhi ya Libya, kila mmoja ameteuwa tume ya kijeshi ya wanachama watano kuwawakilisha katika mazungumzo yaliyoanza jumatatu iliyopita mjini Geneva lengo likiwa kufikia makubaliano imara zaidi ya kuweka chini silaha.
Akifiifisha matumaini Salame ameyataja mazungumzo hayo yanaofanyika kwa daraja ya maafisa wa ngazi ya juu kuwa "hayana mfano."Lakini msitarajie kila kitu kitapatiwa ufumbuzi kufumba na kufumbua" amesisitiza.
Mazungumzo yanafanyika baada ya kusogezwa mbele
Amesema lingekuwa jambo la maana zaidi kama pande hizo mbili zingeketi pamoja na kuanza kuzungumza.
"Pande hizi mbili zinaonyesha kiu cha kutaka kuketi pamoja na kuzungumza" amesema amjumbe huyo maalum wa umoja wa mataifa akiddhirisha kwamba hadi wakati huu mazungumzo si ya ana kwa ana.
Mazungumzo haya ya Geneva yalikuwa yaanze january 28 iliyopita, lakini yalishindikana kwasababu kukataa kushiriki mazungumzoni wawaakilishi wa jenerali Khalifa Haftar.
Mjumbe huyo wa Umoja wa mataifa alilazimika kwenda Benghazi ,mashariki mwa Libya ,jumatano iliyopita ili kuonana na kumtanabahisha Khalifa Haftar hadi alipokubali kutuma ujumbe mazungumzoni mjini Geneva.