Lebanon bado kwafukuta
31 Oktoba 2019Mwandamanaji mmoja ambaye pia ni mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Zena amesema wamekubaliana kufungua barabara kuu lakini watakuwa tayari kuzifunga tena iwapo raisMichel Aoun hataunda serikali mpya mapema iwezakanavyo.
Rais Aoun anatarajiwa kuhutubia umma baadae hii leo katika maadhimisho ya miaka mitatu tangu kuchaguliwa kwake. Kulingana na katiba rais anatakiwa kuitisha mashauriano na bunge kama sehemu ya mchakato wa kumpata waziri mkuu mpya.
Duru zilizo karibu na Aoun zimelidokeza shirika la habari la DPA kwamba majadiliano hadi sasa yanaelekea kumtaja tena waziri mkuu aliyejiuzulu Saad al-Hariri kuunda serikali mpya.
Waandamanaji wanasema bado wataendelea kubaki mitaani kwa kuwa bado kuna mahitaji ambayo wanataka watimiziwe. Wanataka serikali mpya ihusishe wasomi badala ya serikali ya kitaifa inayohusisha vyama vyote vya kisiasa ili kusaidia kufufua uchumi uliozorota pamoja na kukabiliana na ufisadi.
Ingawa wana maoni tofauti kuhusu kurejea kwa Hariri bado wapo wanaotaka kurejea kwake kutokana na uzalendo, hasa kufuatia hatua yake ya kujiuzulu ili kuepusha madhara zaidi. Anwar Aloosh alisema "Naunga mkono Hariri aunde serikali ya mpito. Nimekuwepo hapa tangu mwanzo na Saad Hariri anajulikana kwa uzalendo, na hasa kwa maamuzi yake ya mwisho ya kujiuzulu, ili mtu yoyote asiwasogelee waandamanaji, lakini pia ahadi zake alizotoa kwamba mtu yoyote asimuumize mwandamanaji." Alisema Aloosh.
Wanajeshi hii leo wameonekana wakijaribu kuondoa vizuizi vya barabarani huku waandamanaji wakiwa bado mitaani. Shule zilitarajiwa kufunguliwa baada ya kufungwa kwa takriban wiki mbili za maandamano lakini jana jioni wazazi walipokea ujumbe mfupi uliosema shule hizo zitaendelea kufungwa kwa sababu za kiusalama.
Wabunge wa upande wa Hezbollah wamesema kujiuzulu kwa Hariri kunaweza kuchelewesha utekelezaji wa mageuzi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaonekana kuwa ni muhimu katika kuinusuru Lebanon na mzozo wa kiuchumi.
Kwenye hotuba kupitia televisheni, iliyosomwa na mmoja wa wabunge wa kundi hilo wamesema mashauriano ya bunge yanatakiwa kuanza, ili kuanzisha mchakato wa kuunda serikali mpya.
Ufaransa imeitaka Lebanon ambayo ni koloni lake la zamani kuunda serikali mpya haraka. Waziri wa mambo ya nje Jean-Yves Le Drian amesema kwenye taarifa yake kwamba hatua hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa Lebanon ili iweze kuongoza utekelezaji wa mageuzi hayo mapya ambayo watu wanayahitaji.