1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Le Pen kuchuana na Macron katika duru ya pili ya uchaguzi

Sylvia Mwehozi
11 Aprili 2022

Rais wa Ufaransa anayetetea kiti chake Emmanuel Macron atakabiliana na mpinzani wake mwenye siasa za mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen katika duru ya pili ya uchaguzi utakaofanyika Aprili 24.

https://p.dw.com/p/49kQ4
Frankreich | Erste Runde der Präsidentschaftswahlen 2022 | Marine Le Pen und Emmanuel Macron
Picha: Paulo Amorim/IMAGO

Macron mwenye umri wa miaka 44 ameongoza katika duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili akifuatiwa kwa karibu na Le Pen ambaye anawania kiti hicho kwa mara ya tatu. Lakini wakati Macron alipoibuka na ushindi mnono katika uchaguzi wa mwaka 2017 na kumfanya kuwa rais mwenye umri mdogo wa Ufaransa, safari hii hana uhakika wa ushindi mzito.

Kulingana na kura zilizokwisha hesabiwa, Macron amepata asilimia 27 akifuatiwa na Le Pen aliyejizolea asilimia 24, huku mgombea mwenye siasa kali za kushoto Jean-Luc Melenchon akiibuka nafasi ya tatu na asilimia 22.

Frankreich | Erste Runde der Präsidentschaftswahlen 2022 | Jean-Luc Melenchon
Mgombea wa urais aliyeshika nafasi ya tatu Jean-Luc MelenchonPicha: Michel Spingler/AP Photo/picture alliance

Akihutubia wafuasi wake jana jioni, Macron alionya kwamba "kinyang'anyiro hakijaisha" na kwamba kampeni zitaamua mustakabali wa Ufaransa na Ulaya. "Nataka kuwashawishi katika siku zijazo, kwamba mradi wetu utajibu kwa uthabiti zaidi kuliko ule wa mrengo wa kulia uliokithiri, hofu zao na changamoto za nyakati. Nitegemeeni mimi."

Kwa upande wake Le Pen ambaye anatafuta kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Ufaransa alisema kuwa.

"Watu wa Ufaransa wamezungumza na kunipa heshima ya kufuzu kwa duru ya pili dhidi ya rais anayeondoka. Kwa mamilioni ya wapiga kura walioniamini, nataka kutoa shukrani zangu za dhati kabisa. Ninachukua jukumu hili kikamilifu na unyenyekevu. Naona matumaini."

Kampeni zafikia ukingoni Ufaransa

Utafiti wa kura za maoni unaonyesha kuwa mchuano katika duru ya pili utakuwa mkali. Taasisi ya Ifop imetatabiri kuwa Macron huenda akapata asilimia 51 na Le Pen asilimia 49 katika duru ya pili. Matokeo ya uchaguzi huo yatakuwa na ushawishi mpana wa kimataifa wakati Umoja wa Ulaya ukijaribu kushughulikia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Macron ameunga mkono vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi wakati Le Pen amekuwa na wasiwasi juu ya athari zake kwa maisha ya Wafaransa.

Ili kushinda duru ya pili ya uchaguzi, wagombea hao wawili watapaswa kuwashawishi wapiga kura waliowaunga mkono wagombea wengine 10 wa urais walioshindwa katika duru ya kwanza. Wagombea wengine wakuu wamekubali kushindwa, isipokuwa mgombea mwingine wa mrengo mkali wa kulia, Eric Zemmour.  Wote wamewataka wapiga kura kuzuia siasa kali za mrengo wa kulia  kushika mamlaka katika duru ya pili.