Macron ashika madaraka kamili
14 Mei 2017Kutawazwa kwake ni mara ya kwanza kwa taifa hilo lenye kushika nafasi ya tano kwa kuwa na nguvu kubwa za uchumi duniani na mwanachama muasisi wa Umoja wa Ulaya kumtawaza mwanagenzi mwenye umri wa miaka 39 ambaye miaka mitatu iliopita alikuwa hajulikani sana na umma na yuko nje ya makundi ya kisiasa yanayotambulikana.
Mtaalamu huyo wa zamani wa uwekezaji wa mabenki anakuwa kiongozi wa Ufaransa mwenye umri mdogo kabisa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha baada ya vita nchini humo na wa kwanza kuzaliwa baada ya mwaka 1958 wakati Rais Charles de Gaulle alipoanzisha utawala wa tano wa Jamhuri ya Ufaransa.
Kauli yake ya kwanza akiwa madarakani amejikumbusha kampeni kali ya uchaguzi ambapo aliweza kumshinda kiongozi wa chama cha National Front wa sera kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen lakini umewakatisha tamaa takriban nusu ya wapiga kura milioni 47 nchini Ufaransa.
Watu wengi wanahisi wameporwa na utandawazi wakati ajira za viwandani nyingi zikihamia nchi za nje na wahamiaji na dunia inayobadilika kwa haraka vikitia kiwingu hisia yao ya utambulisho wa Ufaransa.
Kuondokana na mgawanyiko
"Mgawanyiko na mipasuko katika jamii yetu lazima iondoke.Najuwa kwamba Wafaransa wanategemea mengi kutoka kwangu.Hakuna kitakachonizuwiya kutetea maslahi makuu ya Ufaransa na kufanya juhudi za kuleta upatanishi wa Ufaransa."ametangaza Macron.
Tafauti na wagombea wengine wa urais mtetezi huo wa Umoja wa Ulaya ameongeza kusema "Dunia na Ulaya zinaihitaji Ufransa kuliko wakati mwengine wowote ule kabla,Ufaransa itakayokuwa madhuhuti inayosema kwa sauti kubwa kuhusu uhuru na mshikamano."
Ataanzisha juhudi zake za kuimarisha uhusiano na Ujerumani ambayo ni nanga ya Umoja wa Ulaya hapo Jumatatu ambapo atakuwa na mazungumzo na Kansela Angela Merkel mjini Berlin na anatarajiwa kushinikiza ujumbe wake kwamba umoja wa Ulaya uko thabiti licha ya kujitowa kwa Uingereza katika umoja huo na wimbi la misukosuko ya fedha na wahamiaji mambo yaliochochea kuongezeka kwa sera kali za mrengo wa kulia.
Waziri mkuu mpya
Hapo Jumatatu anatarajiwa kutangaza jina la waziri mkuu wa taifa hilo ambaye kazi yake itakuwa ni kusimamia mageuzi nafuu ya rais yenye lengo la kupunguza kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira na kufufuwa uchumi unaozorota.Lakini waziri mkuu huyo itabidi aidhinishwe na bunge la Ufaransa baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa bunge mwezi ujao.
Iwapo chama kingine kitajinyakulia wingi wa viti, atapaswa kumtaja waziri mkuu miongoni mwa wabunge wa chama hicho na kutakuwa na hatari ya kupoteza udhibiti katika ajenda za siasa za ndani.
Polisi 1,500 wamemwagwa kuhakikisha usalama wakati wa kutawazwa kwa Macron huku sehemu kubwa ya mji wa Paris ikiwa imefungwa kwa usafri wote wa magari wakati wa asubuhi.
Mwandishi : Mohamed Dahhman/ Reuters/dpa
Mhariri : Sudi Mnette