Kwenya kuwanunulia wafugaji mifugo baada ya mafuruko
19 Aprili 2023Kupitia mamlaka ya kitaifa ya kukabiliana na majanga nchini humo NDMA, serikali inatarajiwa kuzinunulia takribani familia elfu 1,200 mifugo.
Baada ya kukamilika kwa tathimini kuhusu hasara iliyotokana na mafuriko iliyoendeshwa na kamati inayoangazia majanga jimboni hapa, imebainika kuwa zaidi ya familia elfu moja zilipoteza mifugo yake iliyosombwa na mafuriko yapata wiki tatu zilizopita.
Waathiriwa wa mafuriko Marsabit wapewa chakula cha msaada
Kwa mujibu wa mratibu wa mamlaka ya kukabiliana na majanga NDMA jimboni hapa Mustapha Parkolo, mafuriko yaliyoripotiwa katika maeneo ya Horr Kaskazini na Moyale yalisababisha hasara kubwa kwa jamii za wafugaji.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa kuangazia majanga hapa Narsabit, Parkolo ameifahamisha kamati hiyo kwamba serikali inalenga kuzindua mpango wa kuwanunulia mifugo wafugaji waliopoteza mifugo yao.
"Tutawanunulia wafugaji mifugo ili kuwasaidia waliopoteza mifugo yao wakati wa mafuriko na ukame. Tunazilenga familia mia tatu kutoka kila eneo bunge. Tutatoa mbuzi na kondoo katika familia hizo zipatazo elfu moja na mia mbili wakati kila eneo bunge likitengewa mifugo mia tatu.”
Aidha, afisa huyo wa NDMA ameeleza kwamba serikali itatumia jumla ya shilingi milioni sita za Kenya katika shughuli hiyo itakayowanufaisha wafugaji kutoka maeneo bunge yote ya hapa Marsabit ikiwemo Saku, Laisamis, Moyale na Horr Kaskazini.
Soma pia: Serikali yawatafutia maji wafugaji Kenya
Kulingana na mratibu huyo, NDMA inatazamia kununua mifugo kutoka kwa wafugaji wa Marsabit. Hilo, Parkolo anaamini litasaidia katika kuwezesha mifugo hiyo kustahimili hali ya hewa ya jimboni hapa.
"Tunataka tununue mifugo hao kutoka hapa Marsabit ili tusije tukaleta magonjwa mapya ya mifugo kwa wafugaji wa Marsabit. Tunafanya hivyo ili kuepuka hali ambapo mifugo watalazimika kuchukuwa muda mrefu kuingiliana na hali ya hewa ya upande huu. Lakini kama hatutapa mifugo hao hapa Marsabit, tutalazimika kutafuta kwingine.”
Mafuriko yaliyoripotiwa jimboni hapa kadhalika yamesababisha kuibuka kwa magonjwa ya mifugo wakati idara ya mifugo ya Marsabit ikiendelea na zoezi la kuwachanja mifugo kutoka maeneo yaliyoripoti mafuriko.
Haya yanajiri wakati ambapo wafugaji wa Marsabit wakiendelea kuwarejesha mifugo yao kutoka kaunti jirani walikokuwa wamehamishiwa kufuatia ukame. Mbunge wa Horr Kaskazini Wario Guyo amesema kuwa mvua zinazoshuhudiwa kwa wakati huu jimboni hapa ni bora kwa kupatikana kwa malisho na maji kwa mifugo.
"Kufuatia mvua tuliyopata katika kipindi cha wiki tatu zilizopita tunaona tuna malisho ya kutosha ambayo yatatosheleza mifugo wetu.”
Baadhi ya wakaazi wamekuwa wakiikosoa serikali ya jimbo kwa kushindwa kuwa na mipango ya kuangazia majanga na badala yake kutegemea misaada ya kila mara ambayo si suluhu ya kuduma katika changmoto inayowakabili wakaazi. Michael Kwena, DW Marsabit.