1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waathiriwa wa mafuriko Marsabit wapewa chakula cha msaada

Admin.WagnerD31 Machi 2023

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limeanza kusambaza chakula cha msaada kwa kutumia ndege kwa waathiriwa wa mafuriko ambao vijiji vyao vimekumbwa na mafuriko yaliyoshuhudiwa jimboni Marsabit

https://p.dw.com/p/4PYfc
Kenia Marsabit Pastoralismus
Picha: DW/Michael Kwena

Tangu mvua kubwa ziliposhuhudiwa hapa Marsabit yapata wiki moja iliyopita, bado baadhi ya wakaazi wameshindwa kuondoka katika vijiji vyao kutokana na mafuriko yaliyoripotiwa kwenye maeneo yao.

Hali hiyo imelisukuma Shirika la Msalaba Mwekundu nchini kuanza kutumia helikopta kwa ajili ya kuwapelekea waathiriwa hao vyakula vya msaada.

Kulingana na mratibu wa shirika hilo ukanda wa juu ya mashariki mwa Kenya, Maurice Anyango, familia kadhaa zinahitaji msaada wa chakula na vifaa vingine vya nyumbani baada ya mafuriko kuzisomba nyumba zao.

''Kuna sehemu ambazo hazipitiki kwa sababu barabara zimeharibiwa. Tutaangalia jinsi hali ya anga itakavyokuwa na kuna maeneo tutamabaza chakula kwa kutumia magari...''

Wakaazi kutoka vijiji vilivyoathirika na mafuriko, wanadai kupitia hali ngumu ya maisha kwani hawawezi kutoka nje ya vijiji hivyo kutafuta chakula kutokana na kuharibika kwa barabara inayoviunganisha vijiji vyao na maeneo ambako kuna maduka. Huyu hapa ni mkaazi wa eneo la Obbu.

''Shida yetu kwa sasa ni kuwa, barabara haipitiki na kwa siku kumi na nne hatujafikiwa na msaada kwa sababu ni ndege tu inaweza kutufikia huku.''

Akizungumza akiwa eneo la Dambala Fachana alipoongoza ujumbe wa serikali kuwapa waathiriwa wa mafuriko vyakula, kaimu kamisha wa jimbo hili, David Saruni alieleza kwamba idadi ya watu wasiopungua mia sita wamefungiwa katika takribani vijiji vitano na imekuwa vigumu kuwafikia kwa chakula.

Kamishna huyo akatumia fursa hiyo kuwaraia wakaazi wanaoishi karibu na maeneo yaliyoshuhudia mafuriko hayo, kuchemsha maji ya kunywa kama hatua ya kuzuia magonjwa yanayoweza kuibuka kutokana na uchafu unaosababishwa na mafuriko.

''Kwa sababu ya mafuriko, kuna uwezekano wa mripuko wa magonjwa kama vile kipindupindu na tunawataka wanachi kuchemsa maji ya kunywa...''

Kufikia leo Ijumaa, bado mvua zimeendelea kushuhudiwa kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo hili, huku wakaazi wakiendelea kuomba kupatiwa msaada kutokana na hali inayowakabili sasa.

Michael Kwena, DW Marsabit.