Kweli Angola inahitaji msaada wa fedha?
11 Oktoba 2007Shirika hilo litaitumia wiki nzima kuelezea shughuli zake pamoja na kukusanya misada ya fedha. Mwaka huu fedha zitakazopatikana zimelengwa kutumiwa katika mradi nchini Angola. Aonavyo mwandishi wa uhariri ufuatao hicho ni kiroja .
Angola mnamo mwaka huu pekee ilichuma kitita cha zaidi ya dola bilioni 30 kutokana na biashara yake ya mafuta. Nchi hiyo inanufaika kila mwaka kutokana na bei ya juu ya ma futa na visima vipya katika mwambao wake .Uchumi wa Angola kwa 2007 unakadiriwa kukua kufikia kwango cha zaidi ya 16 asili mia. Kwa wakati huu talari Angola ni mtoaji mkubwa wa pili wa ma futa barani Afrika baada ya Nigeria.
Kweli kwa mtazamo huo nchi hii inahitaji msaada wa fedaha kutoka shirika la kupambana na njaa la kijerumani-Welt Hunger-Hilfe ? Jibu lililo wazi kabisa ni HAPANA.Haiwezekani kwamba umma wa Angola usiweze kunufaika wakati kuna ukuaji wa kiuchumi . Uchumi ni mzuri kiasi cha kuwa hapahitajiki msaada. Kinyume chake lakini inasikitisha kuwa sekta ya jamii iko katika hali mbaya kabisa. Mfano mmoja muhimu ni hali ya watoto na kiwango cha vifo miongoni mwao. Kila mtoto wa nne nchini Angola hufariki dunia kabla ya kufika umri wa miaka 5. Duniani kote n inchini Sierra Leone tu ambako idadi ya watoto wanaofariki ni kubwa zaidi.
Wakati huo huo wasomi na wakubwa wanaishi maisha ya kifahari. Kikundi kidogo na familia ya ya Rais Eduardo dos Santos wamegeuka matajiri wakubwa katika miaka ya karibuni tu. Pamoja na safari zake chache za nje mwaka huu, rais ameagiza ndege kwa gharama ya euro 100 milioni. Ndege hiyo itakua na hata baa ya viburudisho ndani. Kwa upande mwengine lakini hakuna fedha kwa ajili ya mradi wa kusambaza maji na kukarabati mitaro katika mji mkuu Luanda.Mwaka uliopita zaidi ya watu 1.000 walifariki dunia kwa sababu ya kipindupindu.
Kwa maoni ya mwandishi wa uhariri huu, kwa zingatio la utajiri ilionao, Angola inaweza kutatua matatizo yake yenyewe.Kwa mujibu wa shirika la haki za binaadamu `Human Rights Watch` ni kwamba kati ya 1997 na 2002 kiasi ya dola bilioni nne zilitoweka bila ya ufafanuzi. Hizo zingeweza kugharimia miradi ya kijamii kwa kipindi hicho cha miaka mitano.
Hata shirika la fedha la kimataifa limekua likizungumzia juu ya ukosefu wa uwazi kuhusu mapato yanayotokana na mafuta. Kutokana na mtazamo huo ushirikiano wake na Angola umezorota kidogo. Na yule anayeuliza masuali mengi akiwa nchini humo hujikuta matatani. Na hayo ndiyo yaliomkumba mwanaharakati wa kiingereza Sarah Wykes aliyekamatwa na kufukuzwa nchini alipokua akifanya utafiti juu ya fedha zinazotokana na mafuta katika jmimbo la Cabinda zinakoangukia.
Kwa jumla serikali inaonekana kuupa kisogo wajibu wake wa kutatua matatizo ya wananchi wake na hasa vita dhidi ya umasikini. Badala yake inayaachia jukumu hilo mashirika yanayotoa misaada. Miaka zaidi ya mitano ya amani nchini Angola, ni kipindi cha kutosha kwa serikali kutumia mapato makubwa ya utajiri wake kutatua matatizo ya kijamii. Na haihitaji msaada wa fedha wa shirika,kwani ina fedha za kutosha.
Kwa mtazamo wa mwandishi kwa hivyo ni kwamba lingekua jambo la maana sana kama Shirika la Welt Hunger Hilfe lingeizingatia nchi isiyo na uwezo wa fedha na inayoendeshwa vizuri zaidi kiutawala kuliko Angola, na kutuma msaada wa fedha zitakazokusanywa .