1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vipi Ethiopia inamuenzi Mfalme Haile Selassie?

12 Septemba 2024

Haile Selassie, mfalme wa zamani wa Ethiopia, aliondolewa madarakani miaka 50 iliyopita. Mfalme huyo ambaye alifanya urafiki na viongozi wa Marekani, Ulaya na China, ameacha kumbukumbu mesto katika nchi yake.

https://p.dw.com/p/4kYMq
Ujerumani | Haile Selassie, mfalme wa zamani wa Ethiopia ameketi.
Haile Selassie, mfalme wa zamani wa Ethiopia akiwa ameketi alipoitembelea Ujerumani mwaka 1954Picha: privat

Haile Selassie, mfalme wa zamani wa Ethiopia, aliondolewa madarakani miaka 50 iliyopita. Mfalme huyo ambaye alifanya urafiki na viongozi wa Marekani, Ulaya na China, ameacha kumbukumbu mesto katika nchi yake. 

Mnamo Septemba 12, mwaka 1974, Haile Selassie, aliyekuwa mfalme wa mwisho wa Ethiopia, alikutana na ujumbe wa kamati mpya ya kijeshi iliyoundwa inayoitwa Derg, katika kasri lake mjini Addis Ababa. Mkutano huo ulikuwa hatua ya mwisho ya Derg kuuondoa madarakani utawala wa kifalme.

Wawakilishi wa ujumbe huo walimtambulisha Haile Selassie kama "Mfalme" na wakamuomba kwa unyenyekevu ahamie mahali palipotengwa kwa ajili ya afya na usalama wake.

Kupinduliwa kwa Haile Selassie miaka 50 iliyopita kulimaliza utawala wa kifalme Ethiopia.

Asfa-Wossen Asserate, mpwa wa Haile Selassie, ameiambia DW kuwa mfalme huyo alianza kama mwanamageuzi, na aliibadilisha Ethiopia ndani ya utawala wake kutoka nchi ambayo ilikuwa na mizizi katika Zama za Kati kuelekea karne ya 20.

Soma pia:Ethiopia yalionya taifa lolote linalonuia kuvuruga uhuru wa taifa hilo

"Nadhani kumbukumbu yake kuu aliyoiacha itakuwa kwamba alikuwa baba wa elimu ya Ethiopia, kwamba alikuwa mwanzilishi wa chuo kikuu cha kwanza cha Ethiopia, na kwamba elimu ilikuwa mojawapo ya matumaini yake makubwa kwa watu wa nchi yake."

Ethiopia ilipata katiba yake ya kwanza mwaka 1931, lakini ilieleza kuwa ni watoto wa wafalme tu ndiyo wangemrithi. Hewan Semon Marye, profesa na mtaalamu wa historia ya sasa ya kisiasa ya Ethiopia katika Chuo Kikuu cha Hamburg, anasema hilo halikutokea katika historia ya Ethiopia.

Wakati wa utawala wa Haile Selassie, Ethiopia ilianza kujenga mabwawa na barabara, na kuanzisha jeshi la wanamaji, kikosi cha anga na shirika la ndege. Hata hivyo, Hewan anasema mtu angeweza kufikiria hali ya kiuchumi ya nchi ambayo ilidorora kwa muda.

"Mwanzo watu walikuwa na matumaini, lakini huwezi kuwa na taifa zima linalotegemea mauzo ya kahawa na aina fulani ya viwanda vya ngozi."

Alikuwa kiungo muhimu kuanzisha AU

Haile Selassie alikuwa kiongozi anayepinga ukoloni, na alikuwa muhimu katika kuanzisha Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU mwaka 1963, mtangulizi wa Umoja wa Afrika tulionao leo.

Mwanadiplomasia wa zamani wa Ethiopia, Teferra Shawl, ameiambi DW kuwa, Haile Selassie aliwakusanya viongozi 32 wa Afrika wakati huo na kuhakikisha kwamba Addis Ababa inakuwa makao makuu ya umoja wa Afrika, kwa kuwakutanisha kwenye mji huo mkuu wa Ethiopia, kutete demokrasia na ukombozi.

Hewan anasema hadi miaka yake ya mwanzo kama Ras Teferi, Haile Selassie alisafiri Kwenda nje ya nchi mara nyingi kuliko kiongozi mwingine yeyote wa Ethiopia, na kujitenga na mila za zamani.

Kwa nini uwakilishi wa Afrika ni muhimu katika Baraza la Usalama ?

Soma pia:Matumaini ya muungano wa Afrika nzima miaka 50 ijayo

Alizitembelea nchi nyingi za Ulaya, ikiwemo Ufaransa, Uingereza na Italia. Akiwa mfalme alimkaribisha Malkia Elizabeth II na Josip BrozTito wa Yugoslavia.

Pia alimtembelea Mao Zedong wa China mjini Beijing na pia kukutana na marais kadhaa wa Marekani, akiwemo Richard Nixon, Dwight D. Eisenhower, Franklin Roosevelt na John F. Kennedy.

Pia alihudhuria mazishi ya Kennedy, mwaka 1963. Alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya kigeni kuitembelea Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani mnamo mwaka 1954.