Kupanda thamani ya dola kwazusha wasiwasi duniani
18 Aprili 2024Kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kupanda kwa asilimia 10% kwa sarafu ya dola kwenye soko la fedha kutapunguza pato la ndani la taifa katika nchi zinazoendelea kiuchumi kwa asilimia 1.9% baada ya mwaka mmoja, pamoja na athari mbaya za kiuchumi zinazodumu zaidi ya miaka miwili.
Karibu sarafu zote za mataifa ya kundi la G20 yenye uchumi mkubwa na yale yanayoinukia kiuchumi zinashuka thamani dhidi ya dola.
Soma zaidi: Misri yapandisha bei ya mafuta kufuatia kushuka kwa thamani ya sarafu
Sarafu ya Lira ya Uturuki imekuwa ikiongoza kushuka thamani tangu mwanzoni mwa mwaka huu kwa 8.8%; Yen ya Japan imeshuka kwa asilimia 8% na Won ya Korea Kusini imeshuka kwa asilimia 5.5%.
Nchi zilizoendelea na zinazoibuka kiuchumi zimeshuhudia sarafu zikidhoofika kwa kasi, huku dola ya Australia, dola ya Kanada na euro ikishuka kwa asilimia 4.4%, 3.3% na 2.8%.
Kimsingi, sababu kubwa iliyoko nyuma ya kuimarika kwa sarafu ya dola ya Marekani ni kupungua kwa matumaini yaliyokuwepo ya kwamba huenda hivi karibuni Benki Kuu ya Marekani ingelipunguza viwango vya riba.
Sababu za kupanda kwa dola
Faharasa inayofuatilia bei za bidhaa muhimu nchini Marekani (CPI), ambayo ilichapishwa Jumatano (Aprili 17) ilionesha bei zimeongezeka kuliko ilivyotarajiwa katika masoko ya nchini humo, hali ambayo inamaanisha huenda viwango vya juu vya mfumko wa bei nchini Marekani vikashuhudiwa tena.
Na hilo litamaanisha benki kuu haitochukuwa hatua yoyote ya kupunguza riba.
Soma zaidi: Nusu ya makampuni ya Ujerumani yakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi
Pamoja na hayo, kuongezeka kwa msukosuko katika eneo la Mashariki ya Kati kufuatia mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Iran dhidi ya Israel hivi karibuni, kumeiimarisha sarafu ya Marekani kuokana na kuwepo hali ya utulivu ndani ya Mareakani.
Hatimaye, wakati uchumi duniani kote unakabiliwa na ukuaji wa wastani, viashiria vya kiuchumi vya Marekani, kuanzia takwimu za ajira hadi mauzo ya rejareja, vinaendelea kuzidi matarajio.
Athari kwa mataifa yanayoendelea
Nchi zinazoendelea zinakabiliwa na athari mbaya kutokana na kupanda kwa dola, kwa sababu kuongezeka kwa thamani ya sarafu hiyo husababisha ongezeko la riba kwa deni lao linalolipwa kwa dola, hivyo kuwaongezea mzigo wa riba.
Mwanzoni mwa mwaka 2024, wengi waliamini kwamba viwango vya riba vya Marekani vitapunguzwa kufikia mwishoni mwa mwaka. Lakini sasa dola inaonekana kuimarika kwa kasi kuliko ilivyotarajiwa.
Soma zaidi: Pato la taifa Ujerumani kunywea hadi asilimia 0.5 mwaka 2023
Masoko yanayoibukia tayari yako katika hali ya mgogoro.
Mnamo Aprili Mosi, Benki Kuu ya Brazil iliingilia kati soko la fedha za kigeni nchini humo kwa mara ya kwanza tangu Rais Luiz Inacio Lula da Silva aingie madarakani mwanzoni mwa mwaka 2023.
Benki ya Indonesia (BI) imekuwa ikiingilia kati ili kupata sarafu yake ya rupia, ambayo iko katika kiwango cha chini kuwahi kufika katika miaka minne.
Gavana wa benki hiyo, Perry Warjiyo, aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuhudhuria mkutano na Rais Joko Widodo siku ya Jumanne, kwamba benki kuu "daima iko sokoni na itahakikisha kuwa sarafu hiyo ni thabiti."
Benki Kuu ya Uturuki pia ilipandisha kiwango cha sarafu yake kwa 5% hadi 50% mwezi Machi ili kukabiliana na kushuka kwa thamani ya lira na kuongeza kasi ya mfumuko wa bei.
Hofu kwa mataifa yaliyoendelea
Wasiwasi huu sio tu kwa nchi zinazoendelea kiuchumi tu. Japan na nchi zingine zilizoendelea zina hofu kuhusu kuendelea kushuka kwa thamani ya sarafu zao.
Kama anavyoeleza Kota Hirayama, afisa katika kampuni inayoshughulikia masuala ya fedha, SMBC Nikko Securities, "hatari ya kurejea kwa mfumuko wa bei inaongezeka katika nchi zinazoibuka kiuchumi" kwa sababu ya viwango vya ubadilishaji fedha na kupanda kwa bei ya mafuta.
Soma zaidi: Marekani yaishauri Nigeria kuwa na sarafu imara
Kupitia barua kwa wawekezaji, mtaalamu alieleza kuwa kuna uwezekano wa kutoongezeka viwango vya riba, na badala yake wafanye mabadiliko ya sera ya fedha ili kukabiliana kwa muda na kushuka kwa thamani ya sarafu zao.
China, kwa mfano, inatumia uwekaji fedha wake wa kila siku kusaidia Yuan, na baadhi ya benki zinazomilikiwa na serikali zinauza akiba ya dola.
Benki ya Indonesia, taifa linaloinukia kiuchumi, nayo inafanya vivyo hivyo.
Imekusanywa na Wakio Mbogho