Kundi la Hezbollah ladai kuishambulia Israel kwa roketi
16 Mei 2024Kundi la Hezbollah nchini Lebanon linaloungwa mkono na Iran limedai kuvurumisha makombora zaidi ya 60 dhidi ya vituo vya kijeshi vya Israel siku ya Alhamisi kulipiza kisasi mashambulizi ya anga ya usiku kucha yaliyofanywa mashariki mwa nchi hiyo.
Israel yamuuwa kamanda katika shambulizi LebanonKatika taarifa yake Hezbollah imesema imeshambulia kwa makombora maeneo kadhaa ya kijeshi ya Israel katika Milima ya Golan inayokaliwa na Israel.
Mapema leo, vyombo vya habari vya serikali ya Lebanon viliripoti mashambulizi ya anga ya Israel usiku kucha katika eneo la Baalbek, lililo chini ya udhibiti wa Hezbollah, saa chache baada ya kundi hilo kufanya mashambulizi ndani kabisa ya ardhi ya Israel.
Soma pia: Hezbollah yavurumisha maroketi 100 katika milima ya Golan
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mapigano ya mpakani kati ya Israel na kundi la Hezbollah yamesababisha vifo vya takriban watu 413 nchini Lebanon, wengi wao wakiwa wanamgambo lakini pia maelfu ya raia.
Aidha maelfu ya watu wamekimbia makazi yao katika maeneo ya pande zote za mpaka.