1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaBrazil

BRICS kutoa fedha kusaidia waathiriwa wa mafuriko Brazil

15 Mei 2024

Kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi la BRICS limeahidi kutoa dola bilioni moja kwa Brazil ili kuwasaidia waathiriwa wa janga la mvua na mafuriko iliyokumba eneo la kusini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4frH2
Athari ya mafuriko katika jumba la Makumbusho la Kihistoria la Sao Leopoldo kusini mwa Brazil
Athari ya mafuriko katika jumba la Makumbusho la Kihistoria la Sao Leopoldo kusini mwa BrazilPicha: Museu Histórico Visconde de São Leopoldo

Mkuu wa benki ya maendeleo Dilma Rousseff, ambaye ni rais wa zamani wa Brazil ameandika kwenye mtandao wa X kuwa, fedha hizo zitasaidia kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa.

Mafuriko yamesababisha vifo vya watu 149 katika jimbo la Rio Grande do Sul huku watu wengine 124 wakiwa bado hawajulikani waliko.

Soma pia: Viongozi wa kundi la BRICS waafikiana kuongeza wanachama 

Mamlaka imesema zaidi ya watu 600,000 wamelazimika kuziacha nyumba zao kutokana na mafuriko katika miji 400.

Benki ya BRICS - kundi linalojumuisha Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini - imeeleza kuwa itatoa zaidi ya dola bilioni moja ili kulisaidia jimbo la Rio Grande do Sul lililoathirika zaidi na mafuriko na kujenga upa miundombinu mijini na vijijini.

Misaada inaendelea kuwasili katika jimbo hilo huku juhudi za uokoaji zikiendelea kwa karibu wiki mbili sasa.