Viongozi wa kundi la BRICS waafikiana kuongeza wanachama
24 Agosti 2023Uamuzi huo umefikiwa wakati wa siku ya pili ya mkutano wa kilele unaofanyika nchini Afrika Kusini.
Hayo yameelezwa na maafisa wanaohudhuria mkutano huo wa mjini Johannesburg ikiwemo Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Afrika Kusini, Naledi Pandor.
Mwanadiplomasia huyo amesema viongozi wa BRICS, wameridhia kuyakaribisha mataifa mengine ndani ya kundi hilo na tangazo rasmi la hatua hiyo litatolewa kabla ya kufungwa kwa mkutano huo leo Alhamisi.
Miito ya kutanua ukubwa wa kundi la BRICS linaloundwa na mataifa ya China, Brazil, Urusi, India na Afrika Kusini, ndiyo ilitawala ajenda za mkutano huo wa 15 wa kilele.
Duru zinasema karibu nchi 12 duniani zimeomba kujiunga na kundi la BRICS, ambalo hivi sasa linawakilisha nusu ya idadi ya watu duniani na robo ya thamani ya uchumi wa ulimwengu.