Kuna ongezeko la wahamiaji haramu Ulaya 2022
16 Desemba 2022Shirika la ulinzi wa mipaka barani Ulaya, Frontex, limesema idadi ya wahamiaji wanaoingia kwenye mataifa ya kanda hiyo kinyume na sheria imeendelea kuongezeka huku Ugiriki na Italia ndiyo nchi zinazotaabishwa zaidi na wimbi la wahamiaji.
Katika taarifa yake iliyoripotiwa na shirika la habari la DPA, Frontex, imesema katika miezi 11 ya kwanza ya mwaka 2022, karibu wahamiaji 308,000 walivuka mipaka ya mataifa ya Umoja wa Ulaya kinyume na sheria. Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 68 ya wahamiaji walioingia Ulaya katika kipindi kama hicho mwaka 2021.
Frontex imesema mataifa ya Balkan Magharibi ambayo siyo wanachama wa Umoja wa Ulaya ndiyo yanatumika kama lango kwa wahamiaji kuingia kwenye mataifa ya Umoja huo.
Shirika hilo pia limearifu juu ya kuongezeka kwa idadi ya safari za boti zinazowasafirisha wahamiaji kutoka idadi ya safari 63,000 mwaka uliopita hadi safari za boti 98,000 mwaka huu.