1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yaonesha kituo chake cha urutubishaji urani

13 Septemba 2024

Korea Kaskazini imetoa picha za mtambo wake wa kurutubisha madini ya urani kwa mara ya kwanza leo Ijumaa, zikimuonyesha kiongozi Kim Jong Un akiutembelea na kutoa wito wa kuongeza mashine zaidi za urutubishaji.

https://p.dw.com/p/4kZn1
Kim Jong Un wa Korea Kaskazini atembelea taasisi ya silaha za nyuklia
Kim Jong Un akizuru mtambo wa kurutubisha urani.Picha: KCNA via REUTERS

Taifa hilo lililofanya jaribio lake la kwanza la nyuklia mwaka 2006 na liko chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa kutokana na mipango yake ya kuunda silaha zilizopigwa marufuku, halijawahi kuweka wazi maelezo kuhusu kituo chake cha kurutubisha urani.

Vifaa kama hivyo vinazalisha urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu -- ambayo inahitajika kutengeneza vichwa vya nyuklia -- kwa kusokota nyenzo hiyo katika mashine pewa kwa kasi kubwa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kaskazini, Kim alizuru taasisi ya silaha za nyuklia na kituo cha kuzalisha vifaa vya nyuklia vya kiwango cha silaha, bila hata hivyo kutoa maelezo kuhusu eneo wala tarehe ya tukio hilo.

Korea Kaskazini| Kim Jong Un akitembelea taasisi ya silaha za nyuklia
Kim Jong Un akitembelea taasisi ya silaha za nyukliaPicha: KCNA via REUTERS

Ujumbe kwa serikali mpya ya Marekani

Kim "alisisitiza haja ya kuongeza zaidi idadi ya mashine pewa ili kuongeza kasi utengenezaji wa silaha za nyuklia kwa ajili ya kujilinda," vyombo vya habari vya serikali viliripoti, vikichapisha picha za Kim akikagua safu za centrifuges.

Soma pia: Korea Kaskazini yarusha makombora mawili, baada ya nyambizi ya Marekani kuwasili Korea Kusini

Wataalamu wamesema ufichuzi huo wa ghafla wa kituo cha urutubishaji wa urani huenda umekusudiwa kuathiri uchaguzi wa rais wa Marekani mwezi Novemba.

Picha hizo ni "ujumbe kwa utawala ujao kwamba haitawezekana kuiondoa Korea Kaskazini," Hong Min, mchambuzi mkuu katika Taasisi ya Korea ya Muungano wa Kitaifa, aliiambia AFP.