Pyongyang yakosoa luteka za kijeshi zikiongozwa na Marekani
30 Juni 2024Korea Kaskazini imeutaja muungano huo kama "NATO ya Asia" na kuonya kwamba luteka hiyo itakuwa na matokeo mabaya.
Kauli hii inajiri siku moja baada ya mataifa hayo matatu kukamilisha mazoezi ya kijeshi ya siku tatu yaliyojikita katika masuala ya ulinzi wa anga, ufyetuaji wa makombora ya masafa marefu, namna ya kukabiliana na manowari pamoja na mafunzo ya kujilinda mtandaoni.
Wizara ya mambo ya nje ya Pyongyang imesema hivi leo kwamba inashutumu vikali uchochezi wa kijeshi unaofanywa dhidi yake na Korea Kusini. Serikali mjini Seoul ilijibu ukosoaji huo na kusema ni upuuzi na kwamba Korea Kaskazini ndio chanzo kikuu cha mvutano kwenye rasi ya Korea.
Viongozi wa Marekani, Korea Kusini na Japan walikubaliana mwaka jana katika mkutano wao wa kilele kufanya mazoezi ya kila mwaka kama ishara ya umoja katika kukabiliana na vitisho vya nyuklia vya Korea Kaskazini na kuongezeka kwa ushawishi wa China.