Kongo:Kuna haja ya kupitia upya mkataba wetu na China
16 Februari 2023Katika ripoti yake kuhusu makubaliano ya ushirikiano tangu Aprili 2008 kati ya Kongo na makampuni ya Kichina, ofisi ya IGF imebainisha mapungufu kadhaa na kuonya kuwa Kongo haikufaidika hata kidogo na mkataba huo.
Ripoti hiyo iliyotangazwa jana Jumatano mjini Kinshasa inabainisha kwamba mkataba huo uliosainiwa mwaka 2008, ulilenga serikali ya Kongo kuyapatia makampuni ya China amana za hadi dola bilioni 90.
Halafu makampuni hayo yalipaswa kuijengea Kongo miundombinu ya msingi. Lakini ni Wachina ndio walifaidika na sio Kongo.
Soma pia:Watu watano wafariki baada ya kuvuta gesi ya metani, Congo
Jules Alingete, Mkaguzi mkuu wa Fedha amesema Kongo ilipata asilimia 32 ya hisa huku wachina wakibaki na asilimia 68 ya mtaji.
"Makampuni ya Kichina tayari yamepata faida inayokadiriwa kuwa karibu dola bilioni kumi za Kimarekani" Alisema mkuu huyo wa fedha.
Ameongeza kwamba kupitia mkataba huo wa kibiashara Kongo imefaidika na dola milioni 822 katika suala la miundombinu ambayo hata haijaonekana.
Sababu za kupitiwa upya mkataba
Kutokana na mapungufu hayo yaliyoonekana kwenye mkataba wa China ndipo ofisi ya IGF imeomba shirika la kiserikali linalohusika na Ufuatiliaji wa Mikataba na Ushirikiano kati ya Kongo na Washirika wa Kibinafsi kurekebisha mkataba huo.
Cha kusikitisha ni kuona baadhi ya Wakongo walishiriki katika kupora madini ya Kongo.
Soma pia:Rais wa Kongo afanya mazungumzo na kiongozi wa Komoro
Ndivyo alivyoeleza Freddy Idu Shembo, mkurugenzi wa shirika hilo ambae aliahidi kwamba atajishughulika ipasavyo na jambo hilo.
"Wawekezaji hawawezi kuja nchini kwetu na kudai haki tumeona hayo tangu miaka kadhaa iliyopita."
Aliongeza kwamba wawekezaji makini wakija Kongo, walete mtaji na kuheshimu thamani ya kile kinachofanyiwa kazi ili kuwe na uwazi na kuzingatia makubaliano.
"Tunachukua jukumu la kutumia kwa manufaa mahitimisho hayo yote." Alikamilisha kwa kusema.
Ripoti hiyo ya Mkaguzi mkuu wa Fedha za serikali imejiri siku chache baada ya serikali ya Kongo kuamua kuzuia uagizaji wa makampuni ya China ili kulazimisha kujadili upya mkataba huo wa mwaka 2008.