Kongo yaandaa mkutano wa kilele wa misitu barani Afrika
5 Julai 2024Jamhuri ya Kongo imekuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa mazingira barani Afrika, ambapo ajenda kuu imekuwa ni upandaji wa miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na athari zake.
Kulingana na shirika la habari la AFP mkutano huo umehudhuriwa na viongozi sita na ni sehemu ya "Mkakati wa muongo wa Afrika wa kudhibiti ukataji na upandaji wa miti" ulizinduliwa na Rais wa Kongo Denis Sassou Nguesso kwenye mkutano wa mazingira wa COP27 mwaka 2023.
Sassou Nguesso alisema "Mkutano huu huenda ukawa ndio mwanzo wa tafiti na pengine kutoa majibu yanayoweza kuokoa maisha." Ni wazi kwamba kunahitajika hatua.... na kwa ujumla ni nia tu ndio inahitajika na kuongeza juhudi, aliongeza Sassou Nguesso.
"Azimio la Brazzavile" linatarajiwa kuidhinishwa mwishoni mwa mkutano huo wa kilele na wataalamu waliliwasilisha kwa viongozi baada ya kukutana katika mji mkuu wa taifa hilo tangu siku ya Jumanne, ambako pia waliwashirikisha wawakilishi wa jamii za jadi na wataalamu wa kiufundi na fedha.
"Changamoto kubwa iliyopo sasa sio tu inalenga katika kuzuia upotevu wa misitu, bali pia kuirudisha ile ambayo tayari ilipotea na kuanzisha misitu mipya," alisema Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat.
Sassou Nguesso aliungana na viongozi wengine ambao ni pamoja na Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana, Umaro Sissoco Embalo wa Guinea-Bissau, Faustin Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Brice Oligui Nguema wa Gabon na Sahle-Work Zewde wa Ethiopia.