1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo na ICC wamekubaliana kuimarisha ushirikiano

Saleh Mwanamilongo
2 Juni 2023

Serikali ya Kongo na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu,ICC, wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wao katika vita dhidi ya kutoadhibiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

https://p.dw.com/p/4S6oB
Mwendesha mshataka mkuu wa ICC, Karim Khan na waziri wa sheria wa Kongo Rose Mutombo
Mwendesha mshataka mkuu wa ICC, Karim Khan na waziri wa sheria wa Kongo Rose MutomboPicha: Justin Makangara/AA/picture alliance

Makubaliano ya ushirikiano katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kivita yalitiwa saini jijini Kinshasa, mbele ya rais Felix Tshisekedi, kati ya waziri wa Kongo wa sheria Rose Mutombo na Karim Khan mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC. Serikali ya Kongo imesema mkataba huo ni fursa ya kujadili miradi mikuu ya haki katika eneo la Maziwa Makuu.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Khan , alipongeza juhudi ambazo zimefanywa nchini Kongo, lakini anazitaka mamlaka za Kongo kuongeza zaidi juhudi zake kuhusu masuala ya haki, hasa mashariki mwa nchi hiyo.

''Ni lazima tuhakikishe kuwa hizi si ahadi tu za kiimani ambazo hazihisiwi na watu wa nchi hii. Inahitaji nia ya kufanya kazi kwa bidii, kutoa haki, kuzingatia misingi zaidi ya kutoa haki, suluhisho kamili ikiwa ni pamoja na utoaji haki ya mpito, haki ya kimataifa na haki ya kitaifa. Na niko tayari kufanya kazi huko The Hague katika kuzingatia malengo haya endapo tuna uwezo.'', alisema Khan.

''Sio tu uwezo wa kuadhibu wahalifu''

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi
Rais wa Kongo Felix TshisekediPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Kwa upande wake, Rais Felix Tshisekedi alizungumzia visa vya uvamizi kati ya nchi, akimaanisha mzozo kati ya nchi yake na Rwanda. Tshisekedi alihimiza mahakama ya kimataifa kujihusisha na visa vya uhalifu wa kivita.

"Ni muhimu Nchi Wanachama wa mkataba uliounda mahakama ya ICC ziweze kuthibitisha ungwaji mkono wao kwa maadili ya Mahakama, yanayoeleweka hasa kwa kuanzishwa kwa taasisi kandamizi ya mahakama iliyopewa sio tu uwezo wa kuadhibu wahalifu, na washiriki wa uhalifu, lakini pia uwezo wa jumla unaojumuisha kimsingi sekta mbalimbali za mahusiano ya binadamu katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.'', alisema Tshisekedi. 

Katika suala hili, serikali ya Kongo ilikata rufaa nyingine katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC ili kuhakikisha mahakama hiyo inazingatia kile inachokiita uporaji wa kimfumo wa maliasili zake mashariki mwa nchi unaofanywa na wanajeshi wa Rwanda na kundi la waasi wa M23.

Tayari ICC inaendesha uchunguzi mashariki ya Kongo tangu mwaka 2004 na haiko wazi iwapo rufaa mpya itabadili mwelekeo wa mahakama. Taarifa ya Wizara ya Sheria ya Kongo ilieleza kuwa lengo la rufaa hiyo litakuwa kumchunguza na kumfungulia mashtaka yeyote aliyehusika na ukiukaji wa haki za binaadamu kati ya mwaka 2022 na 2023. Kongo imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, ingawa serikali ya Rwanda imekana kuhusika kwa namna yoyote ile.

Ziara ya siku nne ya mwendesha mashtaka wa ICC, Karim Khan, nchini Kongo ilimfikisha Ituri na Kivu Kusini, majimbo mawili yaliyokumbwa na ghasia, na ambayo ililenga kutathmini hali ya haki nchini humo. Siku ya Jumatatu, alikutana na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Dk. Denis Mukwege huko mjini Bukavu, jimboni Kivu ya Kusini.