Kipchoge atamba kwenye mbio za Berlin Marathon
25 Septemba 2023Bingwa mara mbili wa Olimpiki Eliud Kipchoge ameshinda kwa mara ya tano mbio za Berlin Marathon nchini Ujerumani kwa kuandikisha muda wa saa 2, dakika 2 na sekunde 42.
Raia wa Kenya aliyeongoza mbio hizo kutoka mwanzo hadi mwisho amewaambia waandishi wa habari, "Ni mafanikio maalum kushinda mbio za Marathon za Berlin mara tano. Ni ishara ya kazi nzuri niliyokuwa nikiifanya Berlin. Nimeikosa rekodi ya dunia lakini kitu kingine kimeibuka. Mimi ndiye binadamu mwenye kasi zaidi Berlin."
Mkenya mwengine Vincent Kipkemboi aliibuka wa pili kwa kutumia muda wa saa 2, dakika 3 na sekunde 13 wakati Muethiopia Tadese Takele akiridhika na nafasi ya tatu kwa kuandikisha muda wa saa 2, dakika 3 na sekunde 24.
Soma pia: Kenya yaongoza riadha Afrika, yamaliza ya 5 duniani
Wawili hao, Vincent Kipkemboi na Tadese Takele walikuwa wanashiriki kwa mara ya kwanza mbio hizo za Berlin.
Kipchoge sasa ameingia kwenye rekodi kwa kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda mbio za masafa marefu za Berlin mara tano na kuipiku rekodi iliyowekwa na Muethiopia Haile Gebrselassie.
Kipchoge pia anashikilia rekodi ya dunia ya mbio za masafa marefu, rekodi aliyoiweka mwaka 2022 mjini Berlin kwa kutumia muda wa saa 2, dakika 1 na sekunde 9.
Soma pia: Mwanariadha Kipyegon wa Kenya ashinda mbio za mita 1500
Na kwa upande wa akina dada, mwanariadha Tigist Assefa wa Ethiopia alivunja rekodi ya dunia ya wanawake kwa kumaliza kwa muda wa saa 2, dakika 11, sekunde 53 na kushinda tena mbio za Berlin Marathon.
Assefa alishinda mbio hizo mwaka jana kwa kuandikisha muda wa saa 2 dakika 15 na sekunde 37, muda huo ulikuwa wa tatu kwa kasi zaidi kwa upande wa wanawake.