1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi Myanmar asema uasi unatishia kulisambaratisha taifa

9 Novemba 2023

Kiongozi wa Myanmar Myint Swe ameonya leo kuwa taifa hilo limo kwenye hatari ya kusambaratika iwapo jeshi litashindwa kuuzima uasi wa makundi ya kikabila yanayoendesha mapambano kwenye mpaka wa nchi hiyo na China.

https://p.dw.com/p/4YbjH
Kiongozi wa Myanmar U Myint Swe
Kiongozi wa Myanmar U Myint SwePicha: U Aung/Photoshot/Xinhua/IMAGO

Matamshi ya kiongozi huyo wa Myanmar anayeungwa mkono na jeshi yameripotiwa na gazeti la kila siku la nchini Mynamar la Global New Light katika wakati mapigano baina ya jeshi la nchi hiyo na muungano wa makundi ya kikabila yamezidi makali ndani ya muda wa wiki mbili zilizopita.

Rais Myint Swe amesema ikiwa jeshi litazidiwa nguvu na kupoteza uwezo wa kuwadhibiti wapiganaji hao kutoka makundi matatu yaliyoungana, taifa hilo la kusini mashariki mwa bara la Asia litagawika vipande.

Hivi sasa makundi hayo ya MNDAA, TNLA na AA yanayopambana na jeshi lililotwaa madaraka kwa nguvu mwaka 2021, yanasema yamechukua udhibiti wa vituo kadhaa vya kijeshi na kuzuia njia muhimu za biashara kati ya Myanmar na China.