Kiongozi wa Hamas asema mkataba wa amani lazima umalize vita
17 Februari 2024Msimamo huo umetangazwa siku moja baada ya Rais wa Marekani Joe Biden, kutoa wito wa kusitishwa vita kwa muda ili kutoa fursa ya kuachiwa huru kwa mateka na wafungwa.
Mazungumzo ya ngazi ya juu ya kusimamisha vita vya Israel na Hamas yalifanyika wiki hii mjini Cairo, Misri, lakini matokeo yake bado hayajawa wazi.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumamosi, Haniyeh anayeishi nchini Qatar, amesema kundi hilo halitokubaliana na chochote kilicho chini ya usitishaji vita, kuondolewa kwa vikosi vya jeshi la Israel kutoka Gaza, kuondoa mzingiro na kutoa hifadhi salama kwa watu walioyahama makaazi yao.
Jana Ijumaa Rais Biden alitoa wito wa usitishaji wa muda wa mapigano Gaza ili kuachiwa mateka kwa uwezekano wa kubadilishana wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiwa Israel.
Familia za mateka wa Israel zimezidisha mbinyo dhidi ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu, kumtaka afikie mwafaka wa kuwezesha kuachiwa kwao.
Hamas ilichukuwa mateka karibu 250 wakati wa mashambulizi yake ya Oktoba 7, ambapo takribani Waisrael 130 wanaendelea kushikiliwa Gaza kwa mujibu wa maafisa wa Israel. Vita vya Israel kulipiza mashambulizi vimesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 28,858, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.