Kim Jong Un akutana na rais Vladmir Putin nchini Urusi
13 Septemba 2023Kim Jong Un ameahidi ushirikiano wa karibu zaidi na Moscow akisema nchi yake iliyotengwa kimataifa siku zote itakuwa pamoja na Urusi.
Picha zilizotolewa na ikulu ya Urusi zimewaonyesha viongozi hao wawili wakisalimiana katika kituo cha safari za anga za mbali cha Vostochny Cosmodrome. Rais Putin amesema eneo hilo la mkutano limechaguliwa mahususi kwa sababu serikali yake inapanga kuisadia Korea Kaskazini katika miradi yake ya setalaiti.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin na kiongozi wa Korea kaskazini, Kim Jong Un wafanya mazungumzo
Katika ziara hiyo Kim Jong Un amefuatana na maafisa wake wa kijeshi wa ngazi za juu akiwemo afisa wa cheo cha juu kabisa cha Marshal, katika jeshi la ulinzi la Korea Kaskazini, Pak Jong Chon pamoja na mkurugenzi wa idara ya sekta ya utengenezaji risasi, Jo Chun Ryong.
Wakati kiongozi huyo wa Korea Kaskazini akiwa Urusi, nchi yake imefanya majaribio ya makombora mawili ya masafa marefu, kwa mujibu wa jeshi la Korea Kusini.