Korea Kaskazini na Urusi kuimarisha uhusiano wao
13 Septemba 2023Mkutano huo umefanyika katika kituo cha kisasa zaidi nchini Urusi cha urushaji wa zana za anga za juu katika eneo la mashariki ya mbali la Vostochny. Kim Jong Un amemwambia Rais wa Urusi Vladimir Putin kwenye mkutano wao wa moja kwa moja uliodumu kwa saa mbili kwamba Korea Kaskazini na urusi zitaendelea kuimarisha uhusiano wao.
Shirika la habari la serikali la Urusi,TASS limeripoti kwamba kabla ya viongozi hao kufanya mazungumzo ya moja kwa moja ya pande mbili, walifanya mazungumzo na wajumbe wao na kisha rais wa Urusi alimwandalia dhifa ya chakula mgeni wake kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un.
Soma:Kim Jong Un: Ziara ya Urusi inaonyesha umuhimu wa kimkakati wa uhusiano wetu
Marekani imeelezea wasiwasi wake kwamba hatua hiyo inaweza kuleta makubaliano ya kupeleka silaha kwa ajili ya vita vya Urusi huko nchini Ukraine. Wataalamu wanasema huenda Urusi ikayatumia mazungumzo hayo kujipatia makombora na vifaru kutoka Korea Kaskazini, nchi ambayo ina kiu ya kupata teknolojia ya hali ya juu ya satelaiti na nyambizi za nyuklia.
Kwa upande wake China imesema, mkutano wa kilele kati ya Kim Jong Un na Vladimir Putin unahusu uhusiano kati ya nchi za Korea Kaskazini na Urusi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Mao Ning ameuambia mkutano wa kawaida wa wanahabari kwamba ziara ya kiongozi wa Korea Kaskazini nchini Urusi ni mpango kati ya nchi hizo mbili.
Mwanzoni haikujulikana viongozi hao wa Urusi na Korea Kaskazini watafanyia wapi mkutano wao na kuliifanya dunia kuingia katika hali ya kubahatisha tu lakini hatimae kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na rais wa Urusi Vladimir Putin amekutana katika kituo hicho cha kurusha roketi huko Siberia. Huo ni mkutano wao wa kilele wa kwanza katika muda wa miaka minne.
AP/RTRE/AFP