1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Haikui chatua Taiwan kikiambatana na upepo mkali

3 Septemba 2023

Kimbunga Haikui kimetua mashariki mwa kisiwa cha Taiwan mapema leo kikiambatana na upepo mkali na mvua kubwa na kusababisha maelfu ya raia kukaa gizani.

https://p.dw.com/p/4VtWj
Mvua zilizoambatana na Kimbunga Haikui zikinyesha Taiwan
Mvua zilizoambatana na Kimbunga Haikui zikinyesha TaiwanPicha: Chiang Ying-ying/AP Photo/picture alliance

Mamlaka nchini humo zilisema Kimbunga Haikui ni dhoruba kubwa ya kwanza kukipiga kisiwa hicho moja kwa moja katika kipindi cha miaka minne.

Takriban watu 4,000 walihamishwa kutoka maeneo hatarishi na biashara kufungwa ili kujiandaa na dhoruba hiyo. Zaidi ya safari za ndege 221 za ndani na 25 za kimataifa zimefutwa huku huduma ya safari za feri nazo zikisitishwa.

Awali, waziri Mkuu wa kisiwa hicho Chen Chien-jen, alikuwa amezihimiza serikali za mitaa kusalia katika tahadhari kubwa ya kukabiliana na maafa yanayoweza kujitokeza. Alionya pia uwezekano wa kimbunga hicho kusababisha maporomoko ya ardhi katika baadhi ya maeneo.