Kim Jong Un ataka jeshi lake lizidishe maandalizi ya vita
10 Agosti 2023Akiwa na sigara mkononi, Kim ameonyeshwa katika ripoti ya shirika la habari la kitaifa la Korea Kaskazini akiwa katika chumba kilichokuwa na wakuu wa jeshi waliovalia sare na akiwa anaotesha kidole katika ramani na picha.
Alikua anajadiliana na wakuu hao wa jeshi hatua kuu za kijeshi dhidi ya Korea Kusini katika mkutano huo wa Tume Kuu ya Kijeshi.
Shirika la habari la Korea KCNA limeripoti kuwa ajenda ya mkutano huo, unaofanyika siku chache baada ya Kim kukagua viwanda vya utengenezaji silaha, ilikuwa ni "suala la maandalizi kamili ya vita" na kuhakikisha kwamba jeshi liko tayari kwa vita.
Uzalishaji silaha kufanyika kwa kiwango kikubwa
KCNA limeripoti bila kutoa taarifa zaidi kuwa katika mkutano huo, kiongozi huyo amemuachisha kazi Pak Su IL na nafasi yake ikachukuliwa na Ri Yong Gil.
Kulingana na mtafiti katika taasisi ya Sejong nchini Korea Kusini, Cheong Seong-chang, huenda ikawa Pak ambaye alipandishwa cheo mwaka jana, ameachishwa kazi kwa kuwa hakuonyesha ueledi katika operesheni za kijeshi.
Cheong ameongeza kwamba huenda ikawa Ri ndiye mtu sahihi katika nafasi hiyo kwa kuwa aliwahi kuishikilia nafasi hiyo kwa muda mrefu.
Ripoti ya shirika hilo la habari imesema kuwa Kim ametoa amri ya viwanda vya utengenezaji silaha kuendelea na uzalishaji mkubwa wa silaha za kila aina, na kutaka silaha hizo zitumike vyema katika luteka za kijeshi.
Mkutano huo pia ulijadili maandalizi ya gwaride kubwa la kuadhimisha miaka 75 ya kuasisiwa kwa Korea Kaskazini mnamo Septemba 9.
Marekani na Korea Kusini kufanya luteka
Afisa katika wizara ya umoja ya Korea Kusini amewaambia waandishi wa habari kuwa, ripoti hii ya shirika la habari la KCNA inaonekana kana kwamba ndio jawabu la Korea Kaskazini kwa mazoezi yajayo ya pamoja ya kijeshi kati ya Korea Kusini na Marekani.
Marekani na Korea Kusini wanajiandaa kwa mazoezi ya pamoja ya kijeshi baadae mwezi huu wa Septemba. Korea Kaskazini inazichukulia luteka hizo za kijeshi kama maandalizi ya uvamizi na imeonya mara kadhaa kwamba hilo ni jambo linaloweza kusababisha jawabu la kivita.
Mwezi uliopita Korea Kaskazini iliandaa gwaride kuu la kijeshi kuadhimisha miaka 70 ya kusitishwa kabisa kwa vita vya Korea. Wachambuzi waliyaelezea maadhimisho hayo kama maonyesho ya Korea Kaskazini ya silaha za nyuklia "makubwa zaidi na yaliyofanywa peupe bila kuficha lolote."
Chanzo: AFP