1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikao cha misaada ya kibinadamu chafanyika Nairobi

Thelma Mwadzaya (Mhariri: Sekione Kitojo)26 Februari 2019

Ajenda kuu inajikita katika umuhimu wa teknolojia katika kutimiza malengo ya dira ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030. Majadiliano pia yamelenga maslahi ya wakimbizi wa ndani na nje.

https://p.dw.com/p/3E7pU
Nairobi Skyline Kenia Stadtansicht
Picha: Fotolia/vladimir kondrachov

Kikao cha 4 cha masuala ya msaada wa kibinadamu na maendeleo AIDF Africa kimefunguliwa jijini Nairobi. Ajenda kuu inajikita katika umuhimu wa teknolojia katika kutimiza malengo ya dira ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 kadhalika changamoto za kuwasilisha misaada ya kibinadamu. 

Kikao hicho cha masuala ya misaada ya kibinadamu kinafanyika barani Afrika kwa mara ya nne. Kwenye hotuba ya ufunguzi rasmi, waandalizi wa AIDF Africa waliweka bayana wanayoyapa kipa umbele wafadhili wa misaada ya kibinadamu na mashirika ya maendeleo. Hoja zilizoibuka ni pamoja na maadili ya kutoa misaada ukizingatia usalama wa wahudumu katika maeneo yenye vita, mahitaji na hali halisi ya wanaopokea misaada, njia mujarab ya kugawa misaada ambayo inapaswa kujumuisha fedha taslimu na mchango wa mashirika ya kijamii.

Majadiliano yalijikita katika maslahi ya wakimbizi wa ndani na nje ukizingatia njia mujarab za kuwatambua na kuwasajili kadhalika kuwalinda na kuwatimizia mahitaji yao. Suala la kuwa na mifumo ya dijitali ya kuwatambua wakimbizi wa ndani na nje lilipewa uzito kwani ni njia moja ya kuwashirikisha kwa karibu zaidi. Mbinu hizo sharti ziambatane na mipango ya serikali za nchi husika wameeleza wataalam kikaoni. 

Majadiliano yamelenga pia maslahi ya wakimbizi, kuwatambua, kuwasajili kadhalika kuwalinda na kuwatimizia mahitaji yao.
Majadiliano yamelenga pia maslahi ya wakimbizi, kuwatambua, kuwasajili kadhalika kuwalinda na kuwatimizia mahitaji yao.Picha: picture-alliance/AP Photo/IOOM/UNHCR/MoMA/B. Bannon

Kulingana na malengo ya maendeleo endelevu ya umoja wa mataifa, azimio la 16 linadhamiria kushajiisha amani katika jamii kwa manufaa ya maendeleo endelevu,kutimiza haki kwa wote na uwajibikaji katika nyanja zote. Moja ya matokeo yake ni kuwa na watu waliosajiliwa kisheria kwa njia halali ifikapo mwaka 2030.

Viashiria vya mikakati hii ni usajili wa watoto walio chini ya umri wa miaka 5 pasina malipo. Inafahamika kuwa ugaidi,uhalifu wa kupindukia na misimamo mikali inachangia katika ukimbizi unaoletwa na umasikini.Pauline Wambeti ni mwakilishi wa shirika la Nuru International nchini Kenya linaloendesha shughuli zake kaunti ya Migori na anaelezea wanavyopambana na uhalifu wa kupindukia kwa kupambana na umasikini.

Ili malengo hayo yatimie, ipo haja ya kuwa na mifumo thabiti ya afya hasa kwa wakimbizi wa ndani na nje. Mitazamo iliyowasilishwa kikaoni iliibua suala la kuwa na uwezekano wa kutumia hela za misaada wa kibinadamu kubadili maisha ya wakimbizi ili kuiondoa hali ya kuwa tegemezi kwa wafadhili. Kikao hicho cha siku mbili pia kilifanikiwa kuwatuza washindi wa tuzo ya mwaka ya mbunifu bora zaidi. Dhamira ni kuupa uhai mpya ushirikiano na ubunifu katika suala zima la kuimarisha maslahi ya wakimbizi na vita dhidi ya umasikini wa kupindukia.