Kesi ya ufisadi dhidi ya Zuma yaahirishwa
17 Mei 2021Zuma anayekabiliwa na msururu wa madai ya ufisadi na ulaghai anakabiliwa na kesi hiyo inayohusiana na manunuzi ya zana za kijeshi zenye thamani ya randi bilioni 30.
Kwenye kesi hiyo, Zuma anakabiliwa na madai16 ya ufisadi kufuatia manunuzi hayo ya ndege za kivita, boti za doria na vifaa vya kijeshi katika makampuni matano ya Ulaya, yaliyokuwa na thamani ya randi bilioni 30 ambayo ni sawa na karibu dola bilioni 2.5.
Akiwa makamu wa rais wa wakati huo Thabo Mbeki, Zuma anatuhumiwa kwa kupokea rushwa ya randi 500,000 sawa na dola 35,000 kwa mwaka kutoka kwa kampuni ya Thales, kuanzia mwaka 1999 ili badala yake aikingie kifua kampuni hiyo dhidi ya uchunguzi wa mikataba, baada ya ufichuzi uliotolewa bungeni. Hata hivyo kampuni hiyo inayakana madai hayo.
Kesi hiyo imeahirishwa mara kadhaa, huku Zuma akiwasilisha mlolongo wa hoja za kufutwa kwa kesi hiyo dhidi yake.
Soma Zaidi: Ramaphosa kutoa ushahidi dhidi ya Zuma
Katika kile kilichoonekana kama pigo la karibuni zaidi mawakili wote wa Zuma walijiuzulu mwezi uliopita bila ya maelezo yoyote. Lakini hata hivyo, wakili wake mpya Thabani Masuku ameiambia mahakama hii leo kwamba Zuma yuko tayari kuendelea na kesi hiyo. "Tunadhani kwamba ni muhimu kwa serikali kutambua kwamba bwana Zuma yuko tayari, na amekuwa tayari kila wakati, na kwamba haipaswi kuchukuliwa kwamba ombi letu ambalo tunakusudia kutoa ni kana kwamba hatuko tayari - tuko tayari ."alisema.
Wafuasi wake waendelea kumkingia kifua.
Nje ya mahakama, Zuma ambaye awali alisema madai hayo yanachochewa kisiasa aliwaambia wafuasi wake waliofurika kwamba si sawa kwa kesi kuendeshwa kwa muda mrefu na madai yakiwa yanabadilika kila wakati. Lakini hata hivyo hakuzungumza zaidi akisema watasema kile wanachotaka kukisema watakapofika mahakamani.
Pamoja na wafuasi hao, maafisa kadhaa wa ANC walifika mahakamani ikiwa ni pamoja na katibu mkuu aliyesimamishwa Ace Magashule ili kuonyesha kumuunga mkono kiongozi huyo wa zamani. Magashule aliliambia shirika la habari la AFP kwamba ameenda kuonyesha mshikamano na Zuma huku akiyapuuza madai hayo akisema kwa kiasi kikubwa yana mrengo wa kisiasa.
Wafuasi wengine wa chama hicho waliovalia fulana za njano na kijani walikuwa nje ya mahakama wakiimba na kupeperusha bendera za chama chaANC. Mmoja ya wabunge wa chama hicho na waziri mkuu wa zamani wa jimbo la North West, Supra Mahumapelo alinukuliwa akisema ni lazima ifike hatua wamruhusu Zuma kupumzika nyumbani kwa amani.
Akiwa mamlakani kati ya mwaka 2009 na 2018, Zuma alishinikizwa na chama chake kujiuzulu kufuatia ongezeko la msururu wa kashfa. Kesi hii inasikilizwa katika wakati ambapo hatua kali dhidi ya ufisadi zikiwa zinatekelezwa na mrithi wake Cyril Ramaphosa aliyeapa tangu alipoingia madarakani kukabiliana vilivyo na ufisadi.
Mashirika: AFPE/RTRE