Kenya yashinda medali mbili za dhahabu London Marathon
21 Aprili 2024Mbio zilizoanza kwa sekunde thelathini za kupiga makofi kwa heshima ya Kiptum, aliyefariki Februari katika ajali ya gari, zilikamilika kwa Mkenya mwenzake na rafiki yake kumaliza katika nafasi ya kwanza.
Mutiso Munyao alitumia muda wa saa mbili, dakika nne na sekunde moja, huu ukiwa ushindi wake wa kwanza katika mashindano makubwa ya marathon.
Mutiso Munyao alisema alizungumza na Kiptum baada ya ushindi wake mjini London mwaka jana na kuwa mshika rikodi huyo wa dunia huwa akilini mwake anaposhiriki mashindano. Muethiopia Kenenisa Bekele mwenye umri wa miaka 41 alimaliza katika nafasi ya pili.
Kenya imeshinda pia medali ya dhahabu, baada ya bingwa wa Olimpiki Peres Jepchirchir alipomaliza wa kwanza katika mbio za wanawake na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea dhahabu yake katika Michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka huu.
Jepchirchir alimpiku mshikilizi wa rekodi ya dunia Muethiopia Tigst Assefa kwa kutumia muda wa saa mbili, dakika 16 na sekunde 16. Mkenya Joyciline Jekposgei alimaliza wa tatu.