Kenya yaagiza chanjo zaidi milioni 30 za corona
12 Mei 2021Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema uamuzi huo umetokana na hatua ya India kutaifisha chanjo aina ya AstraZeneca. Kenya ilikuwa ikiagiza chanjo hizo kutoka India, ambayo sasa inakabiliana na ongezeko la maafa ya ugonjwa wa Covid-19.
Tamko la waziri Kagwe linaibua hofu kwa Wakenya waliokuwa wamepata dozi ya kwanza ya chanjo hiyo aina ya AstraZeneca na sasa walikuwa wanasubiri dozi ya pili na ya mwisho ya chanjo hiyo.
Mataifa mengine 93 ambayo yalikuwa yakiitegemea India kwa chanjo ya Astrazeneca, pia yamelazimika kutafuta njia mbadala ya kupata chanjo huku makali ya virusi vya corona yakizidi kuongezeka huku virusi hivyo vikibadilika. Kufuatia uhaba wa chanjo hizo serikali ya kenya imelazimika kuagiza dozi milioni 30 za chanjo ya Johnson and Johnson. Waziri Kagwe ametoa hakikisho kwa watu waliopata dozi ya kwanza kuwa wasiwe na wasiwasi.
"Hata kama ulipata dozi moja, unaweza ukapata ulinzi wa hadi asilimia 60, ukipata virusi hivyo, changamoto tuliyo nao ni hali inayolikabili taifa la India.”
Kampuni inayotengeza chanjo ya AstraZeneca iliyoko nchini India, imesema haiwezi kutoa hakikisho kwa mataifa yaliyokuwa yameagiza chanjo hiyo. Taasisi hiyo ya Serum, imesema imeanza kurejesha fedha kwa mataifa yaliyokuwa yameshawasilisha maombi yao. Hatua hiyo imesababisha uhaba wa dozi milioni 90 kwa mpango wa Covax, huku watu milioni 40 wakiathiriwa kuanzia Machi na watu wengine milioni 50 mwezi Aprili ulimwenguni kote.
Kwenye mkutano na mawaziri wa Afya barani Afrika, waziri Kagwe alipendekeza fedha zote zilizochangishwa kupitia Covax zitumike kulipia dozi milioni 200 za Pfizer na dozi nyingine 210 zitumike kununua chanjo ya Johnson and Johnson.
Vituo vilivyokuwa vinatoa dozi ya kwanza ya chanjo hiyo aina ya AstraZeneca kwa wakenya vilikuwa vimesema kuwa dozi ya pili ya chanjo hiyo ingetolewa baada ya miezi minane. Hata hivyo serikali ilibadilisha na kusema kuwa ingetolewa mwezi wa sita kutokana na ucheleweshaji wa kusafirisha. Ni wazi kuwa hata sasa huenda waliopata chanjo hiyo wasipate dozi ya pili. Wakenya milioni moja kati ya milioni 50 wameshapata chanjo hiyo. Mpaka sasa wanasayansi hawafahamu athari ya kukosa dozi ya pili ya chanjo hiyo kwa kinga ya mwili.