Kenya: Polisi ahukumiwa kifo kwa kumuua wakili Willie Kimani
3 Februari 2023Maiti za watatu hao zilipatikana zimeshindiliwa kwenye mifuko ya plastiki na kutupwa mtoni kaunti ya Machakos.
Ifahamike kuwa hukumu ya kifo ilitekelezwa kwa mara ya mwisho kiasi ya miaka 30 iliyopita japo bado adhabu hiyo inaendelea kutolewa.
Baada ya miaka isiyopungua sita, hatimaye familia ya wakili Willie Kimani sasa inashusha pumzi. Mnamo Ijumaa katika mahakama kuu nchini Kenya, Jaji Jessie Lessit ambaye sasa ni wa mahakama ya rufaa, aliwapata na hatia ya mauaji na kumhukumu kifo afisa wa polisi Fredrick Ole Leliman kwa mauaji ya wakili huyo na wengine wawili ya mwaka 2016.
Afisa wa polisi Stephen Cheburet amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, mwenzake Sylvia Wanjiku miaka 24 jela na Peter Ngugi aliyekuwa mdakizi atafungwa miaka 20 jela.
Watetezi wa haki wataka uchunguzi Kenya
Watatu hao walitiwa hatiani mwezi Julai mwaka uliopita wa 2022. Jaji Jessie Lessit aliwapata na hatia ya mauaji ya mtetezi wa haki za binadamu Willie Kimani na mteja wake Josephat Mwenda pamoja na dereva wa teksi Joseph Muiruri waliopoteza maisha tarehe 23 mwezi wa Juni mwaka 2016.
Bi Rebecca Mwenda ambaye ni mjane wa marehemu Josephat Mwenda na alidondoka na kuzirai alipojaribu kuzungumza na waandishi wa habari baada ya hukumu kutangazwa.
Kwa upande mwengine, mahakama iliipa uzito hoja kuwa ushuhuda wa Peter Ngugi uliwasaidia wachunguzi.
Ushuhuda wake ndio uliomnasa afisa Fredrick Leliman kwani aliungama na kuwaelezea wachunguzi kuwa Willie Mwenda na Muiruri waliuawa kinyama.
Kufuatia hilo, Peter Ngugi aliiomba mahakama asihamishiwe jela nyengine kwa kuhofia usalama wake.
Amekuwa akizuiliwa kwenye jela ya Naivasha wakati kesi ilikuwa ikiendelea na anaripotiwa kubadili mienendo na kuwa mcha Mungu hivi sasa ni kasisi.
Ifahamike kuwa Kenya ilitekeleza kwa mara ya mwisho hukumu ya kifo zaidi ya miaka 30 iliyopita ijapokuwa bado inaendelea kuitoa adhabu hiyo.Mwaka 2017, mahakama ya juu iliamuru kuwa hukumu ya kifo ya lazima inakiuka katiba.
Kulingana na ripoti mpya ya mradi wa hukumu ya kifo, DPP kwa ushirikiano na tume ya taifa ya kutetea haki za binadamu,KNCHR, kiasi ya wafungwa 600 wamehukumiwa kifo na wanasubiri adhabu hiyo.
Kwa sasa Cliff Ombeta ambaye ni wakili wa maafisa wa polisi Fredrick Ole Leliman na Steven Chebureti ametangaza kuwa atakata rufaa.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya,DW Nairobi.