Kenya kupeleka kikosi cha polisi 600 zaidi Haiti
11 Oktoba 2024Akizungumza Ijumaa na wanahabari katika ikulu ya Nairobi alipokuwa mwenyeji wa Waziri Mkuu wa Haiti Garry Conille, Rais Ruto aliongeza kusema kuwa bajeti ambayo taifa hilo inayo itakidhi mahitaji ya kikosi kilichoko Haiti hadi mwezi Machi mwaka ujao.
Rais William Ruto ambaye amekuwa akipigia debe amanikatika taifa hilo la Carribean, amesema kuwa tangu vikosi vya polisi vitue katika nchi hiyo ambayo imeathiriwa na magenge ya wahalifu, mwanga wa matumiani wa amani umeanza kushuhudiwa.
Ulinzi wa miundombinu na kuboresha mazingira ya kuishi
Hatua ambayo imeanza kurejesha imani ya raia wa Haiti. Rais Ruto alibainisha kwa sasa kikosi cha maafisa 600 wa polisi kinachotarajiwa kuelekea katika taifa la hilo kinafanya mafunzo kabla ya kuondoka.
''Tunayo bajeti ambayo itatusukuma hadi mwezi Machi mwaka ujao. Kwa hivyo kwa misingi ya kuwasaidia polisi wetu pamoja na kikosi kingine kitakachojiunga nao mwezi ujao, tuna rasilimali ambazo zitawafaa hadi mwaka ujao,'' alisema Ruto.
Ruto amesema kuwa maafisa wa Kenya wanashirikiana na wenzao wa Haiti kulinda miundombinu na kujenga mazingira bora ya kuishi.
Rais Ruto amesema hadi kufikia sasa shule kadhaa zimefunguliwa, uwanja wa ndege pamoja na hospitali kwenye himaya za makundi ya kihalifu.
Rais huyo wa Kenya pia amempongeza Rais wa El Salvador, Nayib Bukele, kwa kuunga mkono ujumbe huo na kutoa msaada muhimu.
Aliongeza kuwa atakuwa akishirikiana na Bukele, pamoja na washirika wengine muhimu ikiwemo Marekani, Bahamas na Canada, ili kuimarisha ushirikiano na kuhakikisha mafanikio ya muungano wa vikosi vya usalama.
Msaada mkubwa wa jamii ya kimataifa
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Haiti, Garry Conille ameyataka mataifa wafadhili kutoa rasilimali zaidi ili kuhakikisha kuwa taifa hilo linakuwa thabiti.
"Natoa wito kwa mataifa washirika wetu kutimiza ahadi walizotoa, wahakikishe kuwa misheni hiyo imefadhiliwa kwa ukamilifu, wahakikishe kuwa vikosi vya usalama vina vifaa vya kutosha kutekeleza majukumu yao,” alisema Conille.
Alibainisha kuwa uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa kuongeza muda wa vikosi vya kudumisha usalama nchini humo kwa mwaka mmoja unaashiria msaada mkubwa kutoka kwa jamii ya kimataifa.
Waziri huyo mkuu wa Haiti, yuko nchini Kenya kwa ziara rasmi ya siku nne.
Kenya inaongoza vikosi vya polisi kutoka mataifa mengine kudumisha amani na usalama katika taifa hilo.
Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa liliidhinisha kupelekwa kwa muungano wa vikosi vya kudumisha usalama nchini humo Oktoba mwaka 2023.