Kenya: Jopo lapendekeza hukumu ya kifo iondolewe
31 Julai 2018Wafungwa waliohukumiwa kifo wataweza kukata rufaa, kutumikia kifungo cha nje au kuachiliwa huru kwa kuzingatia mazingira, ikiwa mapendekezo ya jopo maalum linalotathmini utekelezaji wa adhabu ya kifo yatapitishwa.
Jopo hilo linapendekeza pia uhalifu kuwekewa madaraja, kesi kusikilizwa upya, lengo likiwa kumtendea haki aliyedhulumiwa na pia kutoa nafasi kwa mhalifu kujirekebisha.
Jopo hilo la wataalam 15 kutoka idara ya mahakama, magereza, tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu-KNCHR, tume ya mabadiliko ya kikatiba na Kamati ya ushauri kuhusu msamaha lina wajibu wa kutoa ushauri mintarafu hukumu ya kifo ambayo bado haijapigwa marufuku nchini Kenya.
Wataalam hao wanapendekeza mahakama kupewa uwezo wa kutoa adhabu nyengine mwafaka ya kifungo cha maisha badala ya hukumu ya kifo. Kulingana na Joseph Were ambaye ni hakimu katika afisi ya msajili mkuu wa mahakama, ipo haja ya kuwa na adhabu anuai ikiwemo kutumikia kifungo nje baada ya muda Fulani na kuzingatia vigezo maalum.
Takwimu rasmi kutokea magerezani zinaonyesha kuwa watu wasiopungua 800 wamehukumiwa kifo hadi sasa. Itakumbukwa kuwa Disemba mwaka uliopita, wafungwa 2 waliohukumiwa kifo walipata nafasi ya kukata rufaa kesi yao kusikilizwa tena kwa minajili ya kuomba adhabu tofauti.
Hii ilikuwa baada ya mahakama ya juu kuamua kuwa hukumu ya lazima ya kifo inakiuka katiba. Francis Muruatetu na Wilson Mwangi walihukumiwa kifo mwezi machi mwaka 2003.
Wakati wa utawala wa RAIS Mwai Kibaki hukumu hiyo ilipunguzwa makali na kuwa kifungo cha maisha mwaka 2009.James Karumba aliwahi kufungwa kwa miaka 12 jela kwa ujambazi na alipokata rufaa alifanikiwa kuachiliwa huru.
Kulingana na jopo hilo maalum ipo haja ya kuwa na mazingira ya kusikiliza tena kesi za waliohukumiwa kifo. Anne Mary Okutoyi ambaye pia ni mwanachama wa jopo hilo na mkuu wa kitengo cha mageuzi na uwajibikaji katika shirika la kitaifa la kutetea haki za binadamu, KNCHR amesisitiza hoja hiyo.
Kwa mujibu wa katiba, adhabu ya kifo inatolewa kwa makosa ya ujambazi, mauaji, kumlisha kiapo mhusika kwa madhumuni ya kuua na uhaini. Wataalam hao pia wanapendekeza uhalifu uwe na madaraja ili mhalifu aadhibiwe anavyostahili na pia kumrekebisha tabia naye mdhulimiwa aipate haki yake.
Hukumu ya kifo ilitimizwa nchini Kenya kwa mara ya mwisho mwaka 1987.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya
Mhariri: Iddi Ssessanga