1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani amalizia ziara yake nchini Kenya

6 Mei 2023

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Jumamosi amemaliza ziara yake aliyoifanya kwenye nchi mbili za Afrika. Scholz amemalizia ziara hiyo nchini Kenya kwa kukitembelea kituo cha nishati ya joto.

https://p.dw.com/p/4QzBS
Kenia | Bundeskanzler Olaf Scholz in Nairobi
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz leo Jumamosi amemaliza ziara yake aliyoifanya kwenye nchi mbili za Afrika. Scholz amemalizia ziara hiyo nchini Kenya kwa kukitembelea kituo cha nishati ya joto. Kiwanda hicho kilichopo umbali wa kilometa 120 kaskazini magharibi ya mji mkuu Nairobi, ndicho kinachoongoza kwa ukubwa barani Afrika na kina uwezo wa kuzalisha megawati 800 za nishati. Nishati ya joto inatoa mchango mkubwa katika sekta ya nishati nchini Kenya. Kenya ni mshirika mkubwa wa biashara wa Ujerumani kwenye eneo la Afrika Mashariki. Kansela Scholz aliongozana na wafanyabiashara kadhaa wa Ujerumani. Kwenye mazungumzo na mwenyeji wake rais William Ruto, Kansela wa Ujerumani aliisifu Kenya kuwa nchi iliyomo mstari wa mbele katika juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi. Kabla ya kuwasili Kenya Scholz alifanya ziara nchini Ethiopia ambapo alikutana na wajumbe wa Umoja wa Afrika pamoja na viongozi wa serikali ya Ethiopia.