Kansela Scholz na Lapid wajadili mipango ya nyuklia ya Iran
12 Septemba 2022Waziri mkuu wa Israel Yair Lapid kwenye mazungumzo hayo amesisitizia kitisho kinachoibuliwa na Iran iliyojihami na silaha za nyuklia.
Lapid mapema leo amesema kuna umuhimu wa kuchukuliwa hatua za pamoja ili kuizuia Iran kujiimarisha zaidi kwenye mipango yake ya nyuklia, na kuongeza kwamba haitakuwa sawa kujaribu kuyafufua makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa mengine matano yenye nguvu zaidi ulimwenguni ya kuidhibiti Tehran na mipango yake hiyo ya nyuklia.
Soma Zaidi:Marekani, Israel waijadili Iran ikigoma kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia
Kwa upande wake kansela Scholz amesema anakubaliana na waziri mkuu Lapid ya kwamba Iran haitakiwi kuwa na silaha za nyuklia ili kupunguza kitisho cha kikanda.
"Tunakubaliana na Israel kwamba Iran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia. Kwa hili, tuna hakika kwamba makubaliano ya kimataifa yanayofanya kazi juu ya zuio na jukumu la mpango wa nyuklia wa Iran ni njia sahihi ya kusonga mbele. Ninasikitika kwamba Iran bado haijaweza kuja na jibu muafaka la mapendekezo yanayoratibiwa na Ulaya." alisema Scholz.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin baada ya mazungumzo hayo, Lapid hakusita kurudia tena matamshi yake kwamba litakuwa ni kosa kubwa kuufufua mkataba huo. Hii ni ziara yake ya kwanza nchini Ujerumani, akiwa waziri mkuu.
Ujerumani na Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa waliotia saini makubalano hayo ya nyuklia ya mwaka 2015, ambayo mara zote yamekuwa yakipingwa na Israel. Marekani ilijiondoa kwenye makubaliano hayo mwaka 2018, chini ya rais Donald Trump, hatua iliyoifanya Iran kuachana na baadhi ya masharti yaliyokuwa kwenye makubaliano hayo.
Kwenye mazungumzo hayo ya kuyafufua, ambayo Iran imekubali kuweka ukomo wa mipango yake ya nyuklia na badala yake iondolewe baadhi ya vizuizi bado hayajaonyesha kuzaa matunda yoyote.
Viongozi hao wawili aidha walijadiliana masuala ya ushirikiano kwenye ulinzi. Lapid alisema Israel itasaidia ujenzi wa jeshi jipya la Ujerumani na hasa katika eneo la ulinzi wa angani.
Lapid na Scholz baadae walikutana na manusura wa mauaji ya Wayahudi waliotoka na Lapid kutoka Israel ili kutembelea eneo la Wannsee mjini Berlin ambako viongozi wa ngazi za juu wa Nazi walikutana kupanga mwaka 1942 kupanga mauaji ya halaiki ya Wayahudi. Lapid mwenyewe ni mtoto wa manusura wa mauaji hayo.
Mashirika: DW