Kamanda wa Hezbollah auawa katika shambulio la Israel Beirut
21 Septemba 2024Mauaji ya kamanda huyo yameongeza hofu ya kuzuka vita kamili kati ya Hezbollah na Israel.
Kundi la Hezbollah limethibisha kifo cha kamanda huyo na kumsifu kuwa mmoja kati ya viongozi wake muhimu.
Chanzo karibu na kundi hilo kimesema Aqil alikuwa akifanya mkutano na wanachama wa Hezbollah wakati alipouawa.
Soma pia: Jeshi la Israel lashambulia miundombinu ya Hezbollah
Mauaji ya Aqil ni ya pili yanayohusisha makamanda wakuu wa Hezbollah tangu kuanza kwa vita katika ukanda wa Gaza.
Shambulio la Israel mjini Beirut lililofanyika mwezi Julai lilisababisha kifo cha Fuad Shukr, mkuu wa oparesheni wa kundi hilo la wanamgambo.
Katika taarifa, msemaji wa jeshi la Israel IDF Daniel Hagari amesema Aqil, ambaye ni kamanda mkuu katika vikosi vya wanachama wasomi wa Hezbollah wa Radwan, aliuawa pamoja na makamanda wengine wa kundi hilo.