1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lashambulia miundombinu ya Hezbollah

19 Septemba 2024

Israel imeshambulia ngome za wanamgambo wa Hezbollah kusini mwa Lebanon huku kiongozi wa kundi hilo Hassan Narallah akisema Israel imepita mstari mwekundu kwa kutekeleza shambulizi ya kielektroniki dhidi ya kundi lake.

https://p.dw.com/p/4kreP
Lebanon Exploding Devices
Kiongozi wa Hezbollah asema Israel imepita mstari mwekundu kwa kushambulia mfumo wake wa kielektroniki.Picha: Hassan Ammar/AP/picture alliance

Jeshi la Israel limesema limeshambulia usiku kucha, maeneo sita ya miundombinu ya Hezbollah na ghala lao la silaha Kusini mwa Lebanon, eneo ambalo ni ngome kuu ya kundi hilo linaloungwa mkono na Iran. Shirika la habari la Lebanon limeripoti pia mashambulizi ya Israel katika miji mingine.

Kulingana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Lebanon Abdallah Bou Habib, shambulizi dhidi ya uhuru na usalama wa Lebanon ni hatari na hatua hiyo inaweza kuutanua zaidi mgogoro uliopo sasa. Nae Waziri Mkuu Najib Mikati ameuhimiza Umoja wa Mataifa kukemea vita vinavyohusisha teknolojia ya mawasiliano, katika mkutano wa Baraza la Uslama la Umoja wa Mataifa utakaojadili shambulizi la Lebanon.

Mashambulizi mapya ya kielektroniki yaitikisa Lebanon

Baada ya kushambuliwa mfumo wao wa mawasiliano, kiongozi wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah amesema Israel imevuka msitari mwekundu kwa kuripua vifaa vyake vya mawasiliano na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30 huku watu wengine zaidi ya 3000 wakijeruhiwa. Nasrallah amesema Israel inachukua jukumu kubwa katika uchokozi inaouonyesha dhidi ya kundi hilo na kuapa kulipiza kisasi. Kundi hilo limesema wanachama wake 25 waliuwawa katika shambulizi la Jumanne.

Awali msemaji wa Baraza la usalama wa kitaifa wa Marekani John Kirby alisema hawaamini  njia ya kusuluhisha hali katika vita vya mashariki ya kati ni kuongeza nguvu nyengine za kijeshi huku akionya pande zote kujizuwia kuutanua zaidi mgogoro uliopo katika kanda hiyo.  Tayari Iran kupitia Mjumbe wake katika Umoja wa Mataifa amesema nchi hiyo ina haki ya kulipiza kisasi baada ya balozi wake kujeruhiwa katika shambulizi la lebanon linalodaiwa kufanywa na Israel.

Lebanon yapiga marufuku vifaa vya elektroniki katika ndege zake

Lebanon | Walkie Talkies
Lebanon imepiga marufuku vifaa vya kielektroniki kama Pagers na simu za upepo maarufu kama walkie-talkies  katika ndege zake.Picha: Anwar Amro/AFP

Lebanon tayari imepiga marufuku vifaa vya kielektroniki kama Pagers, simu za upepo maarufu kama walkie-talkies  katika ndege zake. Mamlaka ya viwanja vya ndege ya Lebanon imesema abiria wanaotumia ndege zao wanapaswa kuambiwa kabisa kwamba vifaa hivyo havitakikani katika ndege za kuelekea Lebanon hadi mawasiliano mengine yatakapotolewa.

Hezbollah yaapa kulipa kisasi mashambulizi dhidi ya Lebanon

Kwa upande mwengine katika vita vya Israel na Hamas, Kamati ya Umoja wa Mataifa hii leo imeilaumu Israel kukiuka makubaliano kadhaa ya usalama ya kulinda haki za watoto, ikisema operesheni yake ya kijeshi mjini Gaza ni miongoni mwa ukiukwaji mkubwa uliofanywa na taifa hilo katika historia ya hivi karibuni. Mwenyekiti wa kamati hiyo Bragi Gudbrandsson, amesema vifo vya watoto havikubaliki na vinavunja moyo.

Blinken awasili Cairo kuendeleza juhudi za amani Mashariki ya kati

Mamlaka ya Palestina imesema watu zaidi ya 41,000 wameuwawa Gaza tangu kuanza kwa mapigano mnamo Oktoba 7. Watoto 11,355 ni miongoni mwa walioangamia katika vita hivyo  Hata hivyo shirika la habari la Israel limeripoti kwamba nchi hiyo imependekeza mpango mpya utakaosaidia kuwaokoa mateka wanaoshikiliwa mjini Gaza, kuachiwa kwa wafungwa wa Paleszina na mfumo mpya wa uongozi mjini Gaza. Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa juu ya mpango huo.

Vyanzo: afp/ap/reuters