1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Harris aonyesha mwelekeo tofauti juu ya mzozo wa Gaza

26 Julai 2024

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ameashiria mabadiliko makubwa kwenye sera ya Marekani kuhusu vita vya Gaza na kumtaka Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kukamilishe makubaliano ya amani.

https://p.dw.com/p/4ilPA
Washington | Benjamin Netanyahu akiwa Marekani - Mkutano na Kamala Harris
Makamu Rais wa Marekani Kamala Harris akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House, Washington, Julai 25, 2024Picha: Nathan Howard/REUTERS

Kamala Harris aidha amesisitiza kuwa hatosalia kimya kuhusu mateso wanayopitia Wapalestina katika ukanda huo. 

Huku akionekana kutofautiana kabisa na namna Rais anayeondoka Joe Biden alivyoushughulikia mgogoro huo, kwa kuiwekea shinikizo Israel nyuma ya pazia, makamu huyo wa rais alisema baada ya kukutana na Netanyahu kwamba ni wakati wa kumaliza vita vya Gaza ambavyo vimesababisha hasara kubwa na umwagaji damu.

Alisema "Kwa hiyo, kwa kila aliyeomba kusitishwa mapigano, na kila aliyepaza sauti akiomba amani, nimewaona. Nimewasikia. Hebu sasa tufikie makubaliano, ili mapigano yasimame na vita viishe. Na nitaangazia namna itakayotuongoza kufikia suluhu ya mataifa mawili."

Soma pia:Marekani yaelezea wasiwasi kuhusu hali ya kiutu Gaza 

Marekani Washington 2022 | Kamala Harris na Barack Obama
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama na mkewe Michelle, wametangaza kumuunga mkono Harris kuteuliwa kugombea urais kupitia chama cha DemocraticPicha: Chris Kleponis/CNP/ABACA/picture alliance

Harris mwenye umri wa miaka 59, anayepigiwa upatu kushinda uteuzi kupitia chama cha Democratic katika wakati anapoendelea kupata uungwaji mkono wa vigogo na hasa baada ya Rais wa zamani Barack Obama na mkewe Michelle kutangaza kumuunga mkono baada ya Biden kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho, amesema alimuongezea shinikizo Netanyahu kutokana na hali mbaya kabisa ya kibinaadamu inayoshuhudiwa Gaza.

Soma pia: Kamala Harris aungwa mkono kugombea urais Marekani

Kamala agusia kuanzishwa taifa la Palestina

Makamu huyo wa Rais ambaye amekuwa na msimamo mkali dhidi ya Israel tofauti na Biden, kwenye mazungumzo hayo, alizungumzia kuanzishwa kwa Taifa la Palestina na kwa mara nyingine, kumtaka Netanyahu na kundi la Hamas kukubaliana.

Rais Biden, kwa upande wake, alifanya mazungumzo na Netanyahu katika ofisi yake ya Ikulu ya White House na kumtaka akamilishe mara moja makubaliano ya kusitishwa mapigano Gaza, yatakayopelekea vita hivyo kumalizika, hii ikiwa ni kulingana na taarifa kuhusiana na mkutano huo iliyotolewa na White House.

Mikutano hii ya White House inafanyika siku moja baada ya Netanyahu kutoa hotuba kali kwenye bunge la Marekani, ambayo pamoja na mambo mengine aliapa kupata ushindi kamili dhidi ya Hamas.

Soma pia:Uchaguzi wa Marekani: Makamu wa rais Kamala Harris ni nani? 

Biden na Netanyahu baada ya mazungumzo yao walizitembelea familia za mateka wa Marekani wanaozuiwa Gaza, ambao walisema bado wana matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa mateka katika siku zijazo.

Streit ums Land – Eskalation im besetzten Westjordanland
Picha: YLE

Licha ya Biden kuendelea kuisaidia kijeshi Israel tangu shambulizi la Oktoba 7, uhusiano baina ya viongozi hao wawili ni wa shakashaka, hasa kutokana na tabia za Israel kwenye vita hivyo na wasiwasi kwamba hatakubali kuingia kwenye makubaliano.

New Zealand, Canada na Australia wataka mapigano kusitishwa

Netanyahu aidha, atakutana na mgombea kupitia chama cha Republican Donald Trump huko Florida baadae leo.

Canada, New Zealand na Australia aidha wametoa wito mapema leo kwenye taarifa ya pamoja wa kusitishwa mara moja mapigano katika Ukanda wa Gaza, huku wakielezea wasiwasi wao kuhusiana na kuongezeka kwa mzozo kati ya Hezbollah na Israel. 

Sehemu ya taarifa ya mawaziri wakuu wa mataifa hayo imesema, "hali katika Ukanda wa Gaza ni ya kutisha sana. Raia wanateseka sana na hilo halikubaliki na halitakiwi kuendelea. Imeitaka Israel kusikiliza miito ya jamii ya kimataifa na kuikumbusha kwamba chini ya sheria ya kimataifa ya kiutu, raia wanatakiwa kulindwa."