Kagame kuchuana na wagombea wawili katika uchaguzi ujao
7 Juni 2024Mkuu wa Tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi Oda Gasinzigwa ametangaza kupitia televisheni ya taifa kuwa walipokea jumla ya maombi tisa ya wagombea kiti cha urais, lakini orodha ya muda baada ya mchujo imewaidhinisha wagombea watatu katika uchaguzi wa Julai 15 kuwa Paul Kagame wa chama tawala cha RPF, Frank Habineza wa Democratic Green Party na mgombea huru Philippe Mpayimana.
Itakumbukukwa kuwa Habineza na Mpayimana walikuwa pia wagombea pekee walioidhinishwa kuchuana na Kagame katika uchaguzi wa mwaka 2017 ambao wote hao wawili hawakuweza hata kupata asilimia moja ya kura. Orodha ya mwisho ya wagombea ikitarajiwa kutangazwa Juni 14.
Mpinzani na mkosoaji wa Kagame azuiliwa kugombea
Jina la Diane Rwigara kiongozi wa chama cha People Salvation Movement ambaye pia ni mgombea maarufu zaidi wa upinzani na mkosoaji wa wazi wa utawala wa Kagame limeondolewa kwenye orodha hiyo kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita.
Soma pia: Mahakama kuu Rwanda yamzuia Ingabire kugombea uchaguzi wa rais
Alipotangaza rasmi nia yake ya kugombea urais mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, Bi Rwigara mwenye umri wa miaka 42 alikuwa na matumaini:
"Ninapolinganisha changamoto zilizojitokeza mwaka 2017 na zinazoshuhudiwa mwaka huu, naweza kusema ilikuwa vigumu zaidi miaka saba iliyopita. Kwa hivyo ni mabadiliko mazuri na ninatumai hali itaendelea hivi. Lakini haimaanishi kuwa hatujakutana na changamoto zozote, lakini ninapolinganisha na mapambano yetu ya mwaka 2017, naweza kusema kuwa mwaka huu ilikuwa rahisi zaidi."
Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Rwanda imesema imeliondoa jina la Diane Rwigara kwa kuwa hakukidhi vigezo mbalimbali vinavyohitajika kama kuwasilisha nyaraka inayoonyesha kutokuwa na rekodi ya uhalifu, kushindwa kutoa hati inayothibitisha kuwa ana asili ya Rwanda na pia kukusanya jumla ya saini 600 za uungwaji mkono zikiwemo 12 kutoka wilaya nane.
Soma pia:Mkosoaji wa Kagame atangaza ari ya kugombea uchaguzi wa rais
Rwigara alienguliwa katika uchaguzi wa mwaka 2017 kwa tuhuma za kughushi saini za wafuasi wake. Alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa hilo pamoja na kuchochea uasi huku akizuiliwa kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kuachiliwa huru baada ya kutokutwa na hatia mnamo mwaka 2018.
Kagame, amekuwa na ushawishi mkubwa nchini Rwanda tangu yalipomalizika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambayo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 800,000 wengi wao wakiwa ni watutsi.
Soma pia: Paul Kagame: Shujaa au Dikteta?
Rais Kagame amekuwa rais wa taifa hilo dogo la Afrika Mashariki tangu mwaka 2000 na ameshinda chaguzi tatu kwa zaidi ya asilimia 90 ya kura na bila shaka anatarajiwa kushinda tena mwezi Julai. Kiongozi huyo amekuwa akisifiwa kwa kuijenga upya Rwanda lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaishutumu serikali yake kwa vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa kuukandamiza upinzani.
Rwanda itafanya uchaguzi wa rais na wabunge Julai 15 baada ya serikali kuamua mwaka jana kuoanisha tarehe za chaguzi hizo.
(Chanzo: AFP)