1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Julian Nagelsmann anatakiwa Bayern Munich kumrithi Tuchel

16 Aprili 2024

Julian Nagelsmann, ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani na aliyetimuliwa na Bayern mnamo 2023, anatajwa kutakiwa kurejea kuifundisha Bayern Munich ambayo msimu huu imeshindwa kuibeba ndoo ya Bundesliga

https://p.dw.com/p/4erAc
 Julian Nagelsmann
Julian Nagelsmann, Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani ambaye anawindwa na klabu yake ya zamani ya Bayern MunichPicha: Sven Simon/Imago Images

Vyombo mbalimbali nchini Ujerumani vimeripoti kuwa uongozi wa klabu ya kandanda ya Bayern Munich upo katika heka heka za kutaka kumrejesha Julian Nagelsmann klabuni humo kuchukua mikoba ya kocha Thomas Tuchel ambaye ataondoka klabuni humo mwishoni mwa msimu huu.

Julian Nagelsmann, ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani na aliyetimuliwa na Bayern mnamo 2023, anatajwa kuwa mtu sahihi wa kuinoa timu hiyo ambaye msimu huu imeshindwa kulibeba taji la ligi kuu ya Ujerumani, Bundesliga, baada ya kuibuka mabingwa kwa misimu 11 mfululizo.

 Nagelsmann
Julian Nagelsmann, Kocha wa timu ya taifa ya UjerumaniPicha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Soma zaidi. Nagelsmann anataka kujiepusha na "hisia zilizopitiliza"

Wakati duru zikimtaja Julian Nagelsmann kutakiwa mitaa ya Munich, klabu hiyo pia ipo kwenye mazungumzo na winga wake Leroy Sane ya kuongeza mkataba wa kuendelea kusalia kwenye viunga hivyo.

Itakumbukwa kuwa Sane alijiunga na timu hiyo mwaka 2020 akitokea Manchester City ya England  na mkataba wake wa sasa unafikia ukomo mwaka 2025.

“Sifikirii sana kuhusu hilo kwa sasa, nipo humu ndani kwa sasa. Kutakuwa na mawasiliano ya kina zaidi na wale wanaohusika katika wiki chache zijazo,” Sane aliliambia jarida la michezo la Kicker.

 Bayern München
Bayern Munich ipo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba na winga wake Leroy Sane wa kuendelea kusalia klabuni humo.Picha: opokupix/IMAGO

Maamuzi ya Sane kubakia klabuni humo yanadaiwa kuwa yatategemea kocha atakayekuja kuchukua mikoba ya Thomas Tuchel.

Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa inachezwa wiki hii

Mbali na ripoti hizo, usiku wa Jumanne kutarindima mechi za Ligi ya Vilabu Bingwa Barani Ulaya, Champions League, ambapo Borussia Dortmund ya Ujerumani itacheza dhidi ya Atletico Madrid, Dortmund wakiwa wanahitaji ushindi wa udi na uvumba ili kusonga mbele baada ya kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa magoli 2-1 dhidi ya Atletico Madrid.

Soma zaidi. Nagelsmann kocha mpya wa Ujerumani kuelekea Euro 24

Barcelona wanahitaji kuusimamia ukucha ushindi wao wa kwanza wa magoli 3-2 dhidi ya PSG katika mchezo wa marudiano usiku wa Jumanne.

UEFA Champions League - Atletico Madrid / Borussia Dortmund
Borussia Dortmund wanacheza na Atletico Madrid katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya kombe la Ligi ya Mabingwa barani UlayaPicha: Oscar del Pozo/AFP

Hapo Jumatano Bayern Munich inatarajiwa kushuka dimbani kukipiga na Arsenal katika mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, mchezo wa kwanza vilabu hivyo vilitoka sare ya magoli 2-2.

Rais wa Bayern Munich Herbert Hainer anaamini kuwa timu hiyo inaweza kushinda kombe hilo la mabingwa wa Ulaya, kombe pekee ambalo limesalia kwa timu hiyo msimu huu.

Mabingwa watetezi wa kombe hilo, Manchester City watakuwa nyumbani Etihad kumenyana na mabingwa wa mara nyingi wa kombe hilo Real Madrid hiyo hiyo Jumatano, mchezo wao wa kwanza ukiwa ulimalizika kwa sare ya magoli 3-3.