Juhudi za kuokoa mapatano Syria zahamia Urusi
3 Mei 2016Siku moja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kuanzisha juhudi za kuyanusuru mapatano ya kusitisha mapigano yanayotishiwa kuvunjika, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov alitarajiwa kukutana na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Staffan de Mistura mjini Moscow.
Usitishaji mapigano wa miezi miwili uliyoratibiwa na Marekani na Urusi unakabiliwa na kitisho kikubwa kabisaa, na Kerry alisema siku ya Jumatatu kuwa Washington na Moscow zilipiga hatua katika kujaribu kudhibiti umuagaji damu. Kerry alitoa matamshi yanayooashiria kuvunjwa moyo baada ya kukutana de Mistura mjini Geneva, akisema mgogoro umeshindwa kudhibitiwa katika njia nyingi na hilo linatatiza kweli kweli.
Idadi ya wasimamizi kuongezwa
Marekani na Urusi zimekubaliana kuongeza idadi ya wasimamizi wa usitishaji mapigano walioko mjini Geneva, alisema Kerry na kuahidi kufanyakazi katika saa zijazo ili kusitisha vurugu ndani ya Aleppo, ambako watu zaidi ya 250 wameuawa katika wiki nzima ya mapigano makali.
Kerry aliutuhumu utawala wa rais Bashar al-Assad kwa kuzilenga kwa maksudi kliniki tatu na hopsitali kubwa, na kusema shambulio dhidi ya hospitali limevuka mipaka.
"Kwa hivyo, pande zote mbili, upinzani na utawala zimechangia katika machafuko haya, na tunashirikiana kwa karibu katika saa zijazo kujaribu kurejesha usitishaji wa uhasama na wakati huo huo kupandoshe kiwango cha uwajibikaji kitakachoambatana na mchakato wa kila siku wa utekelezaji wa usitishaji mapigano."
Silaha zanyamanza Aleppo
Silaha zilinyamanza Jumatatu jioni, na kuwaruhusu wakaazi kutoka mitaani na wengine wakafungua hata maduka yao. Muuzaji wa mboga Abu Nazem, aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, kuwa "niliamua kurudi kazini kwa sababu sikuweza kufanya kazi wiki nzima iliyopita kwa kuhofia mashambulizi. Lakini licha ya kunyamanza kwa silaha, nasikia sauti za pikipiki na kuanguka chini nikidhani ni ndege za kijeshi."
Waziri Kerry alisema timu ya wasimamizi ilioimarishwa itafuatilia ukiukaji kwa saa 24 kwa siku, na siku saba kwa wiki. Mwanadiplomasia wa juu wa Marekani aliezungumza na kwa sharti la kutotajwa jina, alisema Marekani, Urusi na Umoja wa Mataifa zimepiga hatua mbele kwenye mfumo mpya wa usitishaji mapigano kwa ajili ya Aleppo, lakini makubaliano yalikuwa bado kukamilika.
Kerry alisitiza kuwa lengo ni kuimarisha makubaliano mapana yenye uwezo wa kuhimili majaribu zaidi, lakini aliwaambia waandishi wa habari kwamba hataki kutoa ahadi zisizoweza kutimizwa, baada ya mkutano wake na de Mistura na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir, ambaye nchi yake ina ushawishi kwa makundi makuu ya waasi.
Mazungumzo na Lavrov
Kabla ya kuondoka Geneva kuelekea Washington, Kerry alimpigia simu Lavrov kujadili makubaliano yanayoyumba, na wawili hao walikubaliana juu ya hatua mpya zitakazochukuliwa na Moscow na Washington, ilisema taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Urusi bila kutoa ufafanuzi zaidi.
Wakati ikikubali kinadharia kuunga mkono usitishaji mapigano, Urusi imefanya kidogo kuvizuwia vikosi vya Assad mjini Aleppo, ambako vilifanya mashambulizi mapema Jumatatu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alitoa wito wa mpango wa usitishaji mapigano uliyorfusha kuujumlisha pia mji wa Aleppo kama suala la haraka.
Usitishaji huo ulirefushwa hadi saa saba za usiku siku ya Jumatano katika mkoa wa Gouta Mashariki, na hadi saa saba za usiku wa leo Jumanne katika mkoa wa Latakia, ambao ni gome ya utawala.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Oummilkheir Hamidou