1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry ajaribu kuokoa usitishaji mapigano Syria

Admin.WagnerD2 Mei 2016

Mashambulizi mapya ya anga dhidi ya mji wa Aleppo nchini Syria yameendelea leo(02.05.2016) wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry akichukua juhudi za dharura kuokoa usitishaji mapigano nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1IgMr
John Kerry
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John KerryPicha: picture alliance/AP Images/J. L. Magana

Akiwasili mjini Geneva jana jioni , Kerry alitarajiwa kufanya mazungumzo na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia, lakini kutokuwapo kwa Urusi kunaweka kiwingu katika mazungumzo hayo.

Marekani na Urusi ni wadhamini wa hatua hizo za mazungumzo hayo ya amani ya Syria, na De Mistura ameweka wazi kwamba haoni matumaini ya kupigwa hatua bila ya mataifa hayo kukubaliana.

Schweiz Syrien Friedensgespräche Staffan de Mistura
Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Syria Staffan de MisturaPicha: picture alliance/dpa/M. Trezzini

Lakini Urusi , wakati ikikubali kimsingi kuunga mkono usitisaji mapigano, haijafanya vya kutosha kuyazuwia majeshi ya rais Bashar al-Assad wa Syria kuzunguka mji wa Aleppo , majeshi ambayo yameendelea kushambulia tena leo Jumatatu.

Mamia ya raia wauwawa

Mapigano ya zaidi ya wiki sasa ndani na kuzunguka mji wa Aleppo mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria yamesababisha kuuwawa kwa mamia ya raia na mashambulizi mapya ya anga yameshambulia maeneo yanayoshikiliwa na waasi upande wa mashariki mwa Aleppo mapema leo asubuhi.

Maeneo mengi ya vitongoji , ikiwa ni pamoja na eneo lenye wakaazi wengi la wilaya ya Bustan al-Qasr , yameshambuliwa, kwa mujibu wa mwandishi habari wa shirika la habari la Ufaransa afp katika mji huo wa kaskazini mwa Syria.

Schweiz Syrien Friedensgespräche
Mazungumzo ya amani ya Syria mjini GenevaPicha: picture alliance/dpa/F. Coffrini

"Kile kinachotokea mjini Aleppo ni cha kuchukiza. Ni ukiukaji wa sheria zote za haki za binadamu. Ni uhalifu," amesema waziri wa mambo ya kigeni ya Saudi Arabia Adel al-Jubeir wakati akikutana na Kerry.

"Ni ukiukaji wa makubaliano yote tuliyofikia ," ameendelea, akimshutumu Assad na Urusi ikikiuka makubaliano ya kimataifa ya kuunga mkono amani.

Kerry alichukua tahadhari zaidi katika majibu yake, akifafanua kile Marekani itakachowabana waasi wenye msimamo wa kati kujitenga na wapiganaji wa jihadi wa al-Nusra Front mjini Aleppo.

Kuna mazungumzo mengi yanayofanyika jana, juzi, leo na tunakaribia mahali tunapoweza kuelewana lakini tuna kazi ya kufanya na ndio sababu tuko hapa.

Kisingizio cha utawala wa Assad

Urusi na utawala wa rais Assad wametumia kuwapo kwa kundi la al-Nusra, ambalo halikuwa sehemu ya makubaliano ya tarehe 27 Februari kusitisha mapigano , kama kisingizio cha kuendelea na mashambulizi yao.

Kuna wasi wasi mkubwa kwamba mapigano hayo yataelekeza kuvunjika kabisa kwa makubaliano ya kihistoria ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa baina ya utawala wa Assad na waasi ambao si miongoni mwa makundi ya Jihadi.

München Sicherheitskonferenz Adel al-Dschubeir Saudi Arabien Außenminister
Waziri wa mambo ya kigeni wa saudi Arabia Adel al-JubeirPicha: Getty Images/AFP/T. Kienzle

Siku ya Jumamosi , Urusi ilisema haitayalazimisha majeshi ya Assad kuacha mashambulizi ya anga katika mji huo ulioharibiwa kwa vita kwa kuwa yanalenga makundi ya jihadi ambayo hayamo katika mpango huo wa kusitisha mapigano.

Marekani imepinga madai hayo na jana Jumapili mkuu wa kituo cha Urusi cha uratibu nchini Syria amesema mazungumzo juu ya uwezekano mpana zaidi wa kusitisha mapigano yameanza.

Kiasi ya raia 253, ikiwa ni pamoja na watoto 49, wameuwawa katika pande zote za mji huo uliogawika tangu Aprili 22, limesema shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri:Yusuf Saumu