Juhudi za kuboresha riadha Kenya
10 Mei 2021Mbio za riadha, zimetia fora sana nchini Kenya, hata kuwa kitambulisho cha taifa hilo kwenye mashindano ya olimpiki kimataifa. Lakini usimamizi mbovu, mazingira duni ya mazoezi pamoja na madai ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli ni changamoto zinaoiandama spoti hiyo.
Shughuli za kuchimba na kujenga misingi imara zimeshika kasi kwenye eneo la Kuresoi ambapo kituo cha mazoezi ya raidha kinajengwa kwenye muinuko wa mita 2,800. William Migwe, afisa mkuu wa wizara ya michezo kwenye serikali ya kaunti ya Nakuru anaeleza kwamba kituo hiki kitawasaidia wanariadha nchini na wanaotoka mataifa ya nje. "Tumeridhika kwa kuwa kufikia sasa tumekamilisha asilimia 25 ya mradi huu. Kufikia miezi mitatu ijayo tutakuwa tunakaribia kukamilisha kazi hii. Awamu ya kwanza imetugharimu shilingi milioni 124.”
Wengi wa wanariadha nchini wametatizika kwa muda kwa kukosa vituo vya kufanyia mazoezi, baadhi wakilazimika kufanyia mazoezi katika barabara za umma na mashuleni. Walio na uwezo walifunga safari na kupiga kambi kwenye kaunti zilizo na vituo vya mazoezi.
Kenya inatambulika kimataifa kwa umahiri wake kwenye riadha, ila usimamizi wa michezo hii nchini umetiliwa shaka mara kwa mara. Katika miaka ya tisini na elfu mbili wanaspoti hasa wakaazi wa eneo la bonde la ufa walianza kutambua kwamba wanaweza kukitumia kipaji chao cha riadha kwa tija, kutokana na namna kilivyokuwa kinaingiza hela nzuri, na ndio hapo wengi wakamiminika kwenye fani hiyo.
Ongezeko hili liliibua madai ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli ambayo yamepelekea wananariadha 46 kuwekewa marufuku kati ya mwaka 2015 hadi mwaka 2018. Shirikisho la riadha nchini limebuni sera na mikakati ya kuikabili hali hii.
Ujenzi wa vituo zaidi vya mazoezi vilevile ni muhimu katika kufanikisha spoti hii, ikizingatiwa kuwa baadhi ya wanariadha wanaochipuka hawana uwezo wa kuwajiri makocha binafsi. Kadhalika ujenzi wa miundo mbinu hii una umuhimu katika kuimarisha uchumi wa jamii
Wakio Mbogho, DW, Nakuru.