1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jonathan na fahari ya kushinwa kwa amani

Admin.WagnerD2 Aprili 2015

Kukubali kushindwa kwa amani ni jambo ambalo limekuwa gumu kuzoweleka na wagombea wengi katika chaguzi za Afrika, lakini hatua ya rais wa Nigeria imemuweka kwenye orodha ya wagombea wanaozidi kukumbatia utamaduni huo.

https://p.dw.com/p/1F29F
Nigeria Bildergalerie Staatspräsidenten Goodluck Jonathan
Picha: T. Charlier/AFP/Getty Images

Katika utamaduni wa siasa za majivuno unaochukulia kuondolewa madarakani kupitia sanduku la kura kama jambo la aibu, kukataa kukubali matokeo mara nyingi hupelekea mapambano ya muda mrefu ya mahakamani, mitaani au hata katika mazingira mabaya zaidi ukandamizaji wa kijeshi.

Hivyo rais wa Nigeria Goodluck Jonathan alipokubali ameangushwa na mpizani wake Muhammadu Buhari, kufuatia ushindi wake wa kushangaza katika uchaguzi wa rais uliyofanyikwa mwishoni mwa wiki, alijiunga na orodha ya viongozi wa Afrika, ambao kukubali kwao kuwa mchezo umekiwsha kumekuwa chanzo cha fahari.

Kutoka urais hadi mafichoni: Rais wa Zamani wa Cote di'Voire Laurent Gbagbo baada ya kukamatwa April 2011
Kutoka urais hadi mafichoni: Rais wa Zamani wa Cote di'Voire Laurent Gbagbo baada ya kukamatwa April 2011Picha: picture-alliance/dpa

Hotuba za nadra

"Nawashukuru tena raia wa Nigeria kwa fursa kubwa niliopewa kuongoza taifa hili, na nawahakikishia kwamba nitanedelea kutekeleza majukumu yangu ya rais kikamilifu hadi mwisho wa muhula wangu. Tayari nimemtakia kila jema Jenerali Muhammadu Buhari," alisema rais Jonathan katika hotuba yake ya kukubali kushindwa.

Hotuba kama hizo zilikuwa za nadra katika bara ambalo bado linaendelea kuzowea utamaduni wa mapambano ya uchaguzi ambako mshindi anachukuwa kila kitu, na ambako madaraka yamekuwa yakibadilika kwa mtutu wa bunduki katika mataifa mengi.

Wasomi wamekuwa wakitafakari juu ya sababu za hali hiyo kwa muda mrefu - inaweza kuwa msisitizo katika jamii za asili za Kiafrika kuhusu ufahamu wao wa dhana nzima ya mashindano, au kwamba kupoteza madaraka kunaweza kumaanisha tofauti kati ya kulala kwenye Ikulu na kibandani.

Bila shaka tofauti kubwa ya ushindi wa Buhari, iliyowezesha mabadiliko ya amani kupitia sanduku la kura katika taifa hilo lenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika ilitoa msaada mkubwa. Lakini pia dhana viongozi wanayohitaji kujua wakati unapofika wa kufungasha virago vyao imepata umaarufu zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Rais Abdoulaye Wade (kulia) alikubali matokeo aliposhindwa na Macky Sall (kushoto) mwaka 2011.
Rais Abdoulaye Wade (kulia) alikubali matokeo aliposhindwa na Macky Sall (kushoto) mwaka 2011.Picha: dapd

Somo kutoka kwa waliotangulia

Wakati rais wa zamani wa Cote di'Voire Laurent Gbagbo alipokataa kukubali kushindwa na Alassane Outtara mwaka 2010, na hivyo kuibua upya vita vya wenyewe kwa wenyewe, mmoja wa wapiga kampeni wa juu wa Gbagbo, nyota wa muziki wa reggae Alpha Blondy, alijitokeza hadharani na kumtaka azingatie haki na kukabidhi madaraka

Alikataa kusikiliza na sasa anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya kimataifa mjini The Hague nchini Uholanzi.

Rais wa zamani wa Senegal Abdoulaye Wade, mwaka 2012 alikuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika Magharibi wa wakati huo kukubali matokeo aliposhindwa na waziri mkuu wake wa zamani Macky Sall, na hivyo kupelekea Sall kutamka kwamba mshindi mkubwa ni raia wa Senegal.

Katika eneo la kusini mwa Afrika pia, kumekuwa na wakati ambapo bwana mkubwa aliambiwa na wapigakura kwamba hakuwa tena maarufu - na hivyo laazima akubaliane na hukumu yao.

Rais wa zamani wa Malawi Bakili Muluzi, ambaye alikuwa moja wa waangalizi wa uchaguzi wa Nigeria kupitia Jumuiya ya Madola, aligombea dhidi ya dikteta Hastings kamuzu Banda mwaka 1994 na kufanikiwa kukomesha utawala wake wa miaka 33.

Muluzi aliliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kuwa Banda hakufurahia hatua yake ya kugombea dhidi yake, akimfananisha na mwanawe, lakini hakuwa na la kufanya.

Rais wa kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda anajifaharisha kwa uamuzi wake wa kuondoka madarakani kwa amani mwaka 1991.
Rais wa kwanza wa Zambia Kenneth Kaunda anajifaharisha kwa uamuzi wake wa kuondoka madarakani kwa amani mwaka 1991.Picha: AP

Kiongozi wa kwanza wa uhuru

Novemba mbili mwaka 1991, gazeti la Telegraph la Uingereza liliripoti kuwa rais wa Zambia Kenneth Kaunda amekuwa kiongozi wa kwanza wa uhuru wa taifa linalozungumza Kiingereza kuondolewa madarakani kwa amani baada ya kukubali kushindwa na Fredrick Chiluba katika uchaguzi mkuu.

Moja wa warithi wake Rupia Banda anaelezwa kutokwa na machozi, aliposhindwa na Michael Sata mwaka 2011, alipoliambia taifa kwamba: "Sina kinyongo moyoni mwangu." Namtakia kila la kheri wakati wa muhula wake wa urais. Muda wangu umekwisha, ni wakati kwangu kusema kwaheri." Pengine Dk. Kenneth Kaunda

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman